0
Uongozi wa Mgodi wa Barrick North Mara unaochimba madini ya dhahabu katika mgodi wa Nyamongo uliopo Wilayani Tarime,umedaiwa kupotosha maelezo yaliyotolewa na Halimashauri ya Wilaya ya Tarime namna ya kutoa fidia kwa Wananchi wanaozunguka karibu na maeneo ya mgodi huo.

Akijibu swali la Diwani wa viti maalum Mariam Mkono (CCM) katika kikao cha Baraza la Madiwani,Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime Amosi Sagara alisema Halimashauri hiyo haikuzuia kutolewa malipo ya fidia kwa Wananchi bali ilitoa maelezo namana nzuri ya kufanywa kwa malipo hayo.

Alisema maelezo yaliyotolewa kwa uongozi wa Mgodi wa North Mara ni kuweka utaratibu mzuri wa kufanywa kwa malipo hayo ambayo baadae kuepuka lawama ambazo zinaweza kujitokeza kutoka upande wowote kuhusiana na malipo ambayo yanapaswa kutolewa kutiokana na fidia.

Sagara alisema Halimashuri haiwezi kuzuia utolewaji wa malipo ya fidia kwa Wananchi wake wanaozunguka mgodi huo kutokana na mahitaji ya aridhi ya mgodi bali wametoa muongozo ambao utafanikisha kuweka utaratibu mzuri wa malipo ya fidia na kila upande upate haki yake.

Alisema kama uongozi wa mgodi umetoa taarifa tofauti na iliyotolewa na Halimashauri hiyo katika kufanikisha ulipaji wa fidia ya aridhi kwa Wananchi wanaozunguka mgodi huo watakuwa wamepotosha na wamekwenda kinyume na maagizo yaliyotolewa.

Mwenyekiti huyo wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime aliwataka Wananchi kuwa wastahimilivu katika kipindi hiki ambacho wanaweka utaratibu mzuri wa kufanikisha ulipaji wa fidia ya ardhi na mambo yatakapokamilka kila kitu kitafanyika na mwenye haki stahili atapata haki yake.

"Tumeshakaa na uongozi wa mgodi wa North Mara na kupeana maagizo namna utolewaji wa fidia utakavyokuwa na kuna taratibu za kisheria ambazo zinawekqwa vizuri na pindi mambo yatakapokamilika yatatolewa matangazo kwa Wananchi wenye maeneo kupewa fida zao,"alisema Sagara.

Katika swali lake msingi,Diwani Mariam Mkono alisema katika barua ya tarehe 23/7/2012 iliyotoka katika Halimashauri ya Wilaya ya Tarime kwenda katika mgodi wa North Mara ilidai kuanzia sasa ni Serikali ndio inayosimamia ardhi kwa niaba ya Wananchi.

Alidai sehemu ya barua hiyo inasema Barrick baada ya kuwa na hitaji la ardhi inapaswa kutoa taarifa ya uchukuaji wa ardhi kwa Mkurugenzi wa Halimashauri hali ambayo ilimshangaza Diwani huyo kwa kuwa ardhi ni mali ya Wananchi na Serikali ni waangalizi.

Katika hatua nyingine madiwani wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime wamedai mrahaba unaotolewa na mgodi huo hauendani na mapato ya yanayopatikana kutoka katika mgodi huku baadhi ya Vijiji vinavyozunguka mgodi huo vikikosa fedha zinazotokana na mrahaba.

Walidai Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa apana zaidi kwani licha ya kuwepo na mgodi huo katika Wilaya hiyo bado kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa Wananchi wanaozunguka mgodio huo kwa kukosa haki stahili huku taratibu nyingine zikiwemo za kusomeshwa kwa wanafunzi wanaozunguka mgodi huo zikiwa hazitekelezwi kwa sasa.

Post a Comment