0
Mwalimu wa Shule ya msingi Kinyariri iliyopo Kata ya Buhemba Wilayani Butiama,Ester Nyamung'ona ametishiwa kuuwawa na Wananchi kutokana na Wanafunzi wa shule hiyo kupatwa na ugonjwa wa kuanguka na kudaiwa kuwa yeye ndiye anayewaroga na kuwasababishia matatizo hayo.

Akizungumza na Blog hii,Mwalimu huyo alidai mnamo februari mosi mwaka huu alivamiwa na Wananchi pamoja na mke wa mganga wa kienyeji na kuanza kumpiga huku wakidai kuwa wamepiga ramli na kuonyesha yeye ndiye anayefanya vitendo vya ushirikina na kusababisha matatizo hayo kwa watoto.

Alisema katika tukio hilo la kupigwa kama sio busara za baadhi ya Wananchi waliokuwepo waliotaka kulifanyia kazi suala hilo Wananchi hao wangeweza kumdhuru vibaya na hata kupeleka kupoteza maisha kutokana na hasira walizokuwa nazo.

"Wananchi walioongozwa na mke wa mganga wa jadi ambaye namfahamu kwa jina la Jabir walinivamia wakidai kuwa wamepiga ramli na kuonyesha mimi ndiye ninayewaroga Wanafunzi na kuanguka huku wakiwa wananipiga huku wengine wakidai kutaka kuniua.

"Nimefedheheka sana na suala hili la kunihusisha na imani za Ushirikina na kuamua kunipiga na kunidhalilisha,tayari nimeandika barua kwa Afisa Elimu na kupeleka nakala kwa Mkuu wa Wilaya na Chama cha Walimu Wilaya ya Butiama kuomba uhamisho wa kuondoka katika shule hiyo kutokana na vitisho nnavyopewa,"alisema Mwalimu Ester.

Alisema tatizo la Wanafunzi kuanguka lilianza wiki ya pili baada ya kuanza muhula wa masomo wa mwaka 2013 baada ya kuanguka Wanafunzi wawili na kudai kuwa uchunguzi uliofanywa n madaktari umeonyesha  kuanguka kwa Wanafunzi hao kunatokana ugonjwa wa Nimonia,Malaria pamoja na ukosefu wa lishe bora.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kinyariri Surusi Mnene alisema tatizo la Wanafunzi kuanguka limekuwa likiendelea na kuongezeka ambapo februari 12 Wanafunzi wapatao 12 walianguka na kwenda kutibiwa katika hospitali ya Wilaya ya Butiama.

Alisema ni kweli Mwalimu Ester alitishiwa kuuwawa na kupigwa na Wananchi kutokanana imani za Ushirikina na kudai katika suala hilo la kuanguka kwa Wanafunzi madaktari wameelezea tatizo hilo linatokana na maradhi pamoja na tatizo la lishe.

Akizungumzia tukio hilo,Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Butiama Wanjara Nyeoja alisema wamelipata tukio hilo la kutishiwa na kupigwa kwa Mwalimu na tayari wamechukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa Polisi juu ya usalama wa Mwalimu huyo na kuandika barua kwa muajiri ili aweze kuhama katika shule hiyo.

Alisema (CWT) inalaani tukio hilo alilofanyiwa Mwalimu huyo na kutaka hatua zaidi zichukuliwe na vyombo vya dola juu ya wale wote waliohusika kuingiza suala la imani za kishirikina na kupelekea kutaka kupoteza uhai wa Mwalimu ambaye anafanya kazi ngumu ya kuwafundisha Wanafunzi.

"Cha kwanza tunaomba usalama wa Mwalimu juu ya kutishiwa kwake na kisha hatua nyingine zichukuliwe ikiwa ni pamoja na Mwalimu kupewa uhamisho kutoka katika shule hiyo lakini pia apelekwe katika shule iliyo karibu na makazi yake ili aweze kufanya kazi kwa amani,"alisema Nyeoja.

Post a Comment