0




Timu ya soka ya maafande wa Polisi mara kesho inashuka dimba la kumbukumbu ya karume mjini Musoma kuvaana na timu ya Mwadui kutoka mkoani Shinyanga katika muendelezo wa michezo ya mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza Tanzania Bara.

Polisi Mara inashuka uwanjani ikiwa na furaha iliyopata wiki iliyopita baada ya kuitandika timu ya Pamba ya Mwanza mabao 2-1 katika uwanja huo huku kocha wa timu hiyo Omari Hamisi akitamba kuendeleza ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuisaka ligi kuu msimu ujao.

Akizungumzia mchezo huo,Omari amesema wachezaji wote wa timu hiyo wapo katika hali nzuri tayari kuikabili timu hiyo ya Mwadui kutoka mkoani Shinyanga na hakuna mchezaji yeyote majeruhi katika kikosi chake.

Amesema katika mchezo uliopita licha ya kuibuka na ushindi dhidi ya timu ya Pamba kulikuwa na kasoro ndogo ndogo katika safu ya ushambuliaji baada ya kukosa nafasi kadhaa za wazi na tayari tatizo hilo ameshalifanyia kazi na kutamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Omari amesema wachezaji wote wapo katika ari ya kutaka kuibuka na ushindi katika mchezo dhidi ya Mwadui na wamepanga kujituma zaidi kutokana na kupata mbinu za kutosha kutoka kwa makocha wao na benchi la ufundi na kuongeza kuwa hawatawaangusha makocha,viongozi pamoja na mashabiki wa timu hiyo.

Kwa upande wake,Msemaji wa timu ya Polisi Mara Shomari Binda amesema licha ya timu hiyo kuwa katika nafasi ya nne hadi sasa bado wanayo nafasi ya kucheza ligi kuu msimu ujao pale watakapofanya vizuri katika michezo iliyobaki ya mzunguko wa pili.


Amesema kikubwa kinachohitajika ni kuwa na ushirikiano wa karibu baina ya wachezaji,makocha na wadau wa soka wa Mkoa wa Mara ili kuweka mikakati ya kuibuka na ushindi katika michezo hiyo ya mzunguko wa pili.

Aidha Binda amewaomba mashabiki wa soka kujitokeza kuishangiria timu hiyo kesho katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma ili kuiongezea hamasa timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mchezo huo

Post a Comment