0
 
 Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, imeandikisha ushindi mwingine mkubwa, pale ilipoilaza Indomitable Lions kutoka Cameroon, bao moja kwa bila, katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa mjini Dar es Salaam.

Mbwana Samatta, anayeichezea klabu ya TP Mazembe ya Congo, ndiye aliyeifungia taifa stars bao hilo la pekee na la ushindi kunako dakika ya themanini na tisa.

Hata hivyo Taifa Stars ingelikuwa na mabao mawili lakini Erasto Nyoni alikosa penalti.

Ushindi huo, unajiri wiki kadhaa baada ya Tanzania kuilaza mabingwa wa Afrika Chipolopolo ya Zambia kwa bao moja kwa bila katika uwanja huo huo wa taifa.
  
Beki wa Cameroon, Ngoula Patrick, anayeichezea klabu ya Union Doula, aliunawa mpira, hatua iliyopelekea refa wa mechi hiyo Munyemana Hudu kutoka Rwanda kuamuru penalti ipigwe.

Baada ya dakika za 45, timu hizo mbili, zilikuwa zikitoshana nguvu ya kutofungana bao lolote.

Hata hivyo katika kipindi cha pili, Tanzania ilirejea huku ikifanya mashambulio makali dhidi ya wageni wao lakini juhudi zao hazikuzaa matunda hadi kocha Kim Poulsen alipofanya mabadiliko na kumtoa kiungo wa Simba, Kazimoto, katika dakika ya 56 na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu.

Ulimwengu aliwahangaisha mabeki wa Cameroon na timu hiyo ilionekana kukosa huduma za nyota wake Samuel Eto'o anayeichezea klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi na Alex Song wa Barcelona ya Hispania, ambao walikuwa wakiuguza majeruhi.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 89 ya mechi hiyo.

Kocha wa Taifa Stars, aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha mchezo mzuri na kusema mechi hiyo imewapa motisha zaidi wachezaji wake na wako tayari kwa michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia.

Kocha wa Cameroon, naye Jean Paul Akono, alikiri kuwa vijana hao wa taifa Stars, walionyesha mchezo mzuri wa walistahili kushinda.

Post a Comment