Chama cha walemavu
Mkoa wa
Mara kimeitaka serikali kuhakikisha inawashirikisha walemavu katika vikao
muhimu vya kujadili maendeleo ngazi za vijiji,kata,wilaya na mkoa ili waweze
kupata fursa ya kuwasilisha kero na mahitaji yao kwa serikali.
Mwenyekiti
wa CHAWATA mkoa wa Mara
Yohana Magai alitoa kauli hiyo mjini Musoma katika Mkutano wa watu wenye
Ulemavu juu ya kujadili mapungufu ya utoaji wa haki za binadamu
yaliyomo katika
katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.
Bw. Magai alisema licha ya marekebisho
mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika katiba hiyo ya nchi, bado uwakilishi
wa watu wenye ulemavu katika vikao vya maamuzi unaonekana ama kupuuzwa au
kutopewa kipaumbele jambo ambalo ni kinyume na
mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo imeridhiwa kutekelezwa na
serikali.
Alifafanua kwamba katika vikao vya kujadili
na kutoa maamuzi juu ya mipango ya kimaendeleo kama vile kamati za maendeleo
ngazi za vijiji(VDC),ngazi za kata(WDC),ngazi za wilaya(DDC) na mkoa (RCC)
zinawakilishwa na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa lakini katika
kamati hizo hakuna uwakilishi wa walemavu.
Kwa msingi huo alisema wakati Taifa
likiwa katika mchakato wa kuandika katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi
katika kujitawala, suala la haki mbalimbali za walemavu ukiwemo uwakilishi wa
kundi hilo katika vikao vyenye maamuzi halina budi kupewa kipaumbele ili
kuendana na sheria ya nchi ya watu wenye ulemavu Na 7 ya mwaka 2009.
Kwa
upande mwingine Mwenyekiti huyo wa
CHAWATA mkoani Mara bw. Yohana Magai aliwahimiza walemavu kuendelea
kuibana Serikali katika utoaji wa haki za msingi kwa kundi hilo muhimu
na kuachana na
tabia ya kulalamika pembeni bila kuiambia serikali wajibu wake kwa
walemavu.
Mkutano huo wa siku tatu juu ya kujadili
katiba ya nchi ya mwaka 1977 na unaowashirikisha walemavu wenye matatizo ya viungo
vya mwili toka wilaya za Rorya,Tarime,Serengeti,Bunda,Butiama na Musoma ulifunguliwa
na katibu tawala wa wilaya ya Musoma bi Dora Makinga.
Awali
akifungua Mkutano huo,Makinga alidai watu wanaoishi na Ulemavu wanayo
nafasi ya kusikilizwa mawazo yao hivyo yale yote yatakayojadiliwa katika
Mkutano huo wa siku tatu yanapaswa kusilizwa na kufanyiwa kazi ili
kuwepo na ushirikishwaji wa pamoja katika kila jambo.
Post a Comment
0 comments