0
SERIKALI mkoani Mara imesema taratibu za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere Kwangwa ineendelea vizuri baada ya Shirika la Hifadhi ya Taifa NSSF kukubali kuojenga baada ya maombi ya mkoa wa Mara katika kutaka kumalizika kwa haraka kwa hospitali hiyo ambayo ilianza kujengwa na Wananchi tangu mwaka 1975.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa kikao Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Mara (RCC) ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Mara Gabriel Tuppa katika kikao cha dharura cha Kamati hiyo kilichokuwa na ajenda ya kujadili na kutoa ushauri katika mpango wa Bajeti ya mkoa wa Mara ya mwaka 2013/2014.

Alisema hospitali ya rufaa ya Mwalimu Nyerere ni moja ya kipaumbele cha mkoa wa Mara kutokanana huduma muhimu ambazo zinatarajiwa kupatikana katika hospitali hiyo mara baada ya kukamilika kwake na kusaidia Wananchi wengi wa mkoa huo ambao mara kadhaa wamekuwa wakilazimika kusafirisha wagonjwa kwenda kwenye hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Tuppa alisema NSSF baada ya kukubali ombi la mkoa wa Mara katika kuimalizia hospitali hiyo bado kunamazungumzo baina ya Shirika hilo na Wizara ya fedha kuona namna ambavyo fedha hizo zitarejeshwa na Serikali baada ya kumalizika kwa ujenzi wa hospitali hiyo.

Alisema anaamini mazungumzo hayo yatakwenda vizuri hasa baada ya kuwasiliana na Waziri wa fedha na kudai tayari wataalamu wa Wizara wapo katika mipango na baadae kukutanana watu wa NSSF kuona namna gani kuhakikisha maombi ya mkoa wa Mara yanapita na ujenzi wa hospitali hiyo kuanza mara moja.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Mara alisema kutokana na umuhimu zaidi wa hospitali hiyo,iwapo kutaonekana kuwa na ucheleweshwaji wa mazungumzo mkoa utaamua kutangaza tenda kwa wazabuni kutokana na fedha walizonazo katika mfuko wa hospitali hiyo ili lengo la kuanza mara moja kwa hospitali hiyo liweze kuanza.

"Tayari mkoa unazo shilingi bilioni nne katika mpango wake wa ujenzi wa hospitali hii ya rufaa ya Mwalimu Nyerere endapo kutakuwa nahatua ndefu baina ya NSSF na Wizara itabidi tutangaze tenda lakini naamini maafikiano yatakuwepo baina ya pande hizo mbili na umuhimu wa hospitali hii na kila kitu kitakwenda vizuri,"alisema Tuppa.

Akichangia kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo,Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime Amos Sagara alisema Serikali lazima ione umuhimu wa hospitali hiyo katika kutoa huduma za afya kwa Wananchi na kuto kuwa na muda mrefu wa kuanza kwa ujenzi huo kwa kuwa Wananchi wenyewe kwa kuona umuhimu wa huduma za afya waliamua kuijenga kwa nguvu zao na kufikia hatua kubwa ambayo sasa inapaswa kuungwa mkono na Serikali hasa katika kumuenzi Baba wa Taifa.

Alisema kwa sasa kumekuwepo na hadha kubwa kwa Wananchi kupata huduma zaidi za kiafya katika mkoa wa Mara na kuamua kuweka kipaumbele katika hospitali hiyo hivyo Serikali inapaswa kusaidia na mkoa ili ujenzi wa hospitali hiyo ambayo itakuwa na huduma mbalimbali muhimu iweze kukamilika.

"Mimi naomba ngugu wajumbe wa kikao hiki cha (RCC) tuitishe maombi maalum ya mkoa mzima kutoka kwa viongozi mbalimbali wa madhebu ya dini ili mazungumzo baina ya NSSF na Wizara yaweze kwenda vizuri na kwa haraka ili ujenzi huu uanze haraka na kupunguza hadha ya kimatibabu kwa Wananchi wa mkoa wa Mara,"alisema Sagara.

Hivi karibunui akiwa katika ziara ya kiserikali mkoani Mara,Makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal alisema hospitali hiyo imo katika ilani ya Uchaguzi ya CCM hivyo lazima Serikali itaifatilia na kuona ujenzi wake unaendelezwa na kukamilika kwa muda muafaka.

Post a Comment