0
MWANAMKE mwenye ujauzito wa miezi sita mkazi wa Wilayani Tarime amepigwa na anayedaiwa kuwa mume wake na kisha kufungwa katika zizi la ng'ombe na kumsababishia majera pamoja na maumivu makali yaliyopelekea kukimbia na kutafuta msaada katika vyombo vya kisheria na mashirika ya kutetea Wanawake.

Tukio hilo limelipotiwa katika kituo cha msaada wa kisheria kwa Wanawake na Watoto cha (CWCA) mjini Musoma baada ya mhanga huyo kufika kwa ajili ya kuomba msaada wa kisheria kutokana na manyanyaso ambayo amedai kufanyiwa na mwanaume huyo kila wakati licha ya kuwa walishatengana.

Akizungumza na BLOG HII ,Afisa Mwandamizi wa Shirika hilo Ostack Mrigo alisema tukio la kupigwa kwa Mwanamke huyo lilitokea mwishoni mwa mwezi machi mwaka huu na kumsabababishia mjamzito huyo ambaye jina limehifadhiwa majeraha mwilini mwake kutokana na kufungwa katika zizi pamoja na maumivu makali.

Mume anayedaiwa kumpiga mjamzito huyo aliyefahamika kwa jina la Joseph Mwita (30) imedaiwa alishatengana na Mwanamke huyo aliyezaa nae watoto watano kwa muda mrefu amekuwa na mazoea ya kumpiga mara kwa mara kwa kumfata katika nyumba yake na kumuunganisha vipigo hivyo pamoja na watoto aliyezaa nae.

Mrigo ambaye ni mwanasheria wa Shirika hilo alisema siku ya tukio hilo mume huyo alikwenda katika kikundi cha mwanamke huyo cha kusaidiana na kuchangiana pesa na kuwataka wanakikundi wampe pesa za mwanamke na kukataliwa na ndipo alipoenda nyumbani kwake nakuanza kumshushia kipigo kisha kwenda kumfunga katika zizi la ng'ombe.

Alisema baada ya kufikishiwa tukio hilo ofisini kwao waliamua kumpa msaada mwanamke huyo kwa kufuatilia na kufanikiwa kumkamata mwanaume huyo na kumfungulia kesi ya jinai katika mahakama mjini Musoma na sasa wapo kwenye utaratibu wa kufungua kesi ya madai ya taraka pamoja mgawanyo wa mali kwa kuwa alipomuacha mwanamke huyo hakutoa taraka.

Afisa huyo wa (CWCA) alidai Shirika hilo litahakikisha linatoa msaada wa kisheria kwa Mwanamke huyo kadri itakavyowezekana kwa kuwa mwanaume huyo amekuwa akimnyanyasa mwanamke huyo kama alivyodai mwenyewe na kwa sasa ameamua kutoka Tarime na kurudi kwao Kinesi Wilayani Rorya na bado hali yake haijawa nzuri kutokana na kipigo alichopata.

Mrigo aliongeza kuwa Shirika hilo kwa sasa linaendesha mafunzo ya Haki za Binadamu,Ukatili wa Kijinsia,Sheria na vyombo vya utatuzi wa migogoro Nchini yanayowashirikisha Wanawake na makundi mengine ili kuweza kuzijua haki na kuelewa mahala pa kwenda pale panapotokea matatizo na migogoro ya kisheria.

Alisema mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Shirika la Legal Service Facility yaliyoanza aprili 2 hadi 5 yatasaidia kwa makundi mbalimbali katika jamii yanayokutana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji kuzijua haki zao na kupunguza vitendo vya ukatili vinavyofanywa kwa Wanawake na Watoto ndani ya jamii.

 

Post a Comment