0
DIWANI wa kata ya Buhare katika Manispaa ya Musoma kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) David Katikiro amemjia juu mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome kwa kitendo cha kuwakamata viongozi wa kata yake pamoja na mjumbe wa Serikali ya mtaa na kumvurugia mkutano ambao alikuwa ameuandaa.

Katika kauli yake mbele ya kikao cha baraza la madiwani wa Manispaa ya Musoma,Katikiro alisikitishwa na kukwazwa na kitendo cha Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alihudhulia katika mkutano wake aliokuwa ameundaa kuzungumza na Wananchi  masuala mbalimbali ya kata hiyo likiwemo suala la ulinzi shirikishi na kuwakamata viongozi hao.

Alisema kutokana na kitendo kilichofanywa na DC Msome kilipelekea mkutano wake kuvurugika na hivyo kushindwa kuzungumza na Wananchi ambao tayari walikuwa wamefika katika mkutano huo kujua kile ambacho Diwani alitaka kuzungumza nao kwa kipindi hicho.

Diwani Katikiro alidai alikwazwa na Mkuu huyo wa Wilaya kwa kitendo alichokifanya siku hiyo kwani mara baada ya kuwakamata viongozi hao mkutano ulishindwa kufanyika kwa kuwa kulikuwa na baadhi ya majibu ya maswali ya Wananchi ambayo yalikuwa yanapaswa kutolewa na viongozi ambao aliwakamata na kuondoka nao.

"Mheshimiwa DC pamoja na wajumbe wa baraza nipate kusema sijawahi kukasirika na kukwazwa kama siku ambayo Mkuu wa Wilaya alivuruga mkutano wangu ambao nilipanga kuzungumza na Wananchi ambao wamenichagua ili niwatumikie.

"Hata kama sheria ilimpasa kufanya hivyo kutokana na nafasi yake subira ilihitajika wakati ule maana kuna masuala mbalimbali yalitakiwa kuzungumzwa katika mkutano ule ambao ulivurugwa na Mkuu wa Wilaya,"alisema Diwani Katikiro.

Akijibu hoja ya Diwani huyo,Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome alisema ilimlazimu kuchukua maamuzi ya kuwakamata viongozi hao baada ya kushindwa kusimamia majukumu yao yakiwemo masuala ya ulinzi shirikishi katika kata ya Buhare.

Alisema katika kata hiyo matukio ya mauaji kwa Wanawake yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara huku viongozi hao wakishindwa kusimamia majukumu yao pamoja na kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi utaratibu ambao umeanzishwa katika kila kata za Manispaa ya Musoma.

"Diwani Katikiro hakunitendea haki kwa kunishutumu na kudai nilimkuzwa kutokana na maamuzi niliyoyachukua katika mkutano wake na Wananchi kwa sababu kata yake ndiyo inayoongoza kutokea matukio ya mauaji na hata yeye kama Diwani hakuna hatua zozote alizozichukua lazima tufanye kazi za Wananchi na tuache kulalamika pasipo sababu,"alisema DC Msome.

Aidha madiwani katika kikao hicho cha Baraza lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halimashauri ya Manispaa ya Musoma walimtaka Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuangalia utaribu mzuri wa kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi na kujua iwapo mtu akipata tatizo akiwa katika ulinzi ni namna gani Serikali itakavyo mshughulikia.

Post a Comment