0
WAZABUNI wa ndani katika mkoa wa Mara,wameanza taratibu za kuifikisha serikali mahakamani  kwa madai ya kushindwa kuwalipa deni lao linaodaiwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni mbili.
 
Serikali inadaiwa kiasi hicho cha fedha zinazotokana huduma mbalimbali zilizotolewa na wazabuni wa ndani kukupitia idara ya Magereza katika wizara ya mambo ya ndani ya nchi,vyuo vya ualimu chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na Tamisemi ikiwemo wizara ya afya kupitia vyuo vyake vyake vya Uganga mkoani Mara.
 
Mwenyekiti wa wazabuni mkoani Mara Edward Muhere,ameliambia gezeti hili kwa njia ya simu kuwa deni hilo linadaiwa na wazabuni hao kuanzia mwaka 2009 hadi sasa na Serikali imeshindwa kuonyesha nia ya dhati kulipa deni hilo.
 
Alisema kuwa wazabuni wa mkoa wa Mara,wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali katika taasisi hizo vikiwemo vyakula katika magereza na vyuo hivyo bila ya kulipwa kwa kipindi hicho,hatua ambayo sasa imewafanya wengi wao kufirisika kabisa na wengine kulazimika kuuziwa nyumba zao na taasisi za fedha yakiwemo mabenki baada ya kushindwa kulipa mikopo walikopa kwa biashara hiyo.
 
“Hivi hii serikali sikivu kwa akina nani hasa,sisi wazabuni wa ndani ambao tumeonyesha uzalendo wa hali ya juu wa kutoa huduma kwa mkopo kwa serikali yetu,lakini leo haitulipi haki zetu kama wanavyolipwa wazabuni wa nje,tumevumilia vya kutosha sasa tumechoka ngoja twende mahakamani”alisema Muhere na kuongeza.
 
“Watu tumekopa mitaji benki tena kwa riba kubwa ili kufanya biashara hii,sasa tulio wengi tumefirisika na wengine wamelazimika kuuziwa nyumba zao ili kulipa mikopo ya benki lakini serikali imeshindwa kulipa fedha zetu huku sisi tukinyanyasika kulipa kwa riba je hapa kuna haki kweli…nashauri watendaji wa serikali wasifanye tuichukie serikali ya CCM ingawa tuna imani kubwa na Rais wetu Jakaya Kikwete”alisema.
 
Mwenyekiti huyo wa wazabuni mkoani Mara,alisema wakati wakiandaa taratibu za kuifikisha serikali mahakamani wamekubaliana kusitisha kutoa zabuni kwa taasisi hizo ili kuhakikisha serikali inawatendea haki wazabuni wa ndani kama inawatendea wazabuni wengine wa nje ya nchi.
 
“Baadhi ya viongozi wa wizara wao hawana matatizo kwani wanatambua deni hili tatizo kubwa lipo hazina sasa sijui wanataka hadi sisi tutoe rushwa ndo tulipwe haki zetu za msingi…kwa kweli serikali ijaribu kuwa na huruma na watu wake,hatuwezi kufisika kiasi hiki na serikali ikaendelea kucheka kuwauawa watu wake hii ni hatari kubwa na nchi inayojiita ya utawala bora na ambayo inadai kutenda haki”aliongeza Muhere.
 
Mmoja ya wakuu wa idara katika moja ya moja ya wizara hizo zinazodaiwa ambaye aliomba kutotajwa gazetini,alipopigiwa simu kuthibitisha kama kweli idara yake ni miongoni mwa wadai hao,alikiri kuwa deni hilo lipo lakini tatizo kubwa ni hazina huku siasa pia ikitumika kuchelewesha ulipaji wa madeni hayo.
 
“Ndugu yangu tunatambua tunadaiwa tena si kiasi hicho tu ni kikubwa zaidi kwa nchi nzima,lakini baadhi yao wanalipwa sasa sijui kutokana na mahusiano na wakubwa huko juu,lakini pia hazina ni tatizo kubwa kwa kweli,wanaweza kuifanya serikali katika siku za usoni ikaja kulipa deni kubwa zaidi kama watu hawa wakianza kudai deni lao kwa riba”alisema kiongozi huyo.
 
Mwishoni mwa mwaka jana katibu mkuu wa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi Selestine Gesimba,alipoulizwa kuhusu deni hilo alikiri kuwa wizara yake inadaiwa na kwamba taratibu zinafanyika kwaajili ya kuhakikisha deni hilo linalipwa lakini hadi sasa hakuna kilicholipwa.
 

Post a Comment