0
Jeshi la polisi mkoni Mara limewafikisha Mahakamani askari wake wawili wanaodaiwa kukamatwa na risasi 1050 zinazodaiwa kuibwa kwenye kikosi cha kuzuia na kutuliza ghasia (FFU).

Askari ambao wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mara ni askari aliyekuwa na cheo cha sajenti Michael Reus wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoa wa Mara pamoja na askari mwenye cheo cha koplo Ally Machembe aliyekuwa akifanya kazi Kibaha mkoni Pwani.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,ilielezwa na mwendesha mashitaka wa Serikali Jonas Kaijage mnamo juni mosi mwaka huu majira ya saa ya usiku askari hao walikamatwa kwenye basi la Mohamed Trans linalofanya safari zake kati ya Musoma na Dar es salaam wakiwa katika harakati za kusafirisha risasi hizo.

Ilielezwa Mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na makosa matatu ikiwemo kosa la kula njama za kufanya wizi,kosa la pili kumwibia mwajili wao kwenye kambi ya FFU na kosa la tatu ni kukutwa na risasi 1050 zinazotumika kwenye bunduki ya SMG na SR pasipokuwa na kibali.

Watuhumiwa hao walipelekwa Mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na dhamana ya shilingi milioni 5 na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali.

Kesi ya askari ambao awali walifikishwa katika Mahakama ya kijeshi na kufukuzwa kazi kutokana na kutenda makosa hayo,kesi inayowakabili imepangwa kusikilizwa tena juni 24.

Post a Comment