0

MBUNGE WA JIMBO LA RORYA LAMECK AIRO AKIGUA BAADHI YA MAJENGO KATIKA ZIARA YAKE YA  KUANGALIA SHUGHULI ZA MAENDELEO KATIKA JIMBO HILO





DIWANI wa Kata ya Tai kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Rorya Godfrey Masiroli amesifia jitihada zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo Lameck Airo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kimaendeleo jimboni na kudai ni Mbunge wa vitendo na sio kuongea.

Kauli hiyo aliitoa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge huyo Kijiji cha Sota baada ya ziara ya kukagua shughuli za Maendeleo za Jimbo hilo na kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Majengo iliyopo katika Kata hiyo baada ya kuezuliwa na upepo.

Alisema Mbunge huyo amekuwa ni mwepesi wa kujitoa na kushiriki mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika jimbo na pale yanapotokea majanga amekuwa akifika kwa wakati na kushirikiana na Wananchi ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo.

Masiroli alisema harambee iliyofanywa na Mbunge huyo katika mkutano wa hadhara japo ni ya kushitukiza lakini inaonyesha ni jinsi gani anavyoguswa na Wananchi wa Rorya na kutaka majengo yaliyoezuliwa na upepo yaweze kukamilika na wanafunzi waendelee na masomo.

"Ndugu zangu hii shule ni yetu na wanafunzi wanaosoma hapa ni wetu naungana na mbunge kwa kuchangia shilingi laki moja ili shule hii iweze kukamilika kwa wakati na vijana wetu waendelee na masomo.

"Katika suala shughuli za Maendeleo itikadi za kisiasa tunaweka pembeni na kwa pamoja tunashiriki shughuli za kimaendeleo jambo hili linalofanywa na Mbunge ni jambo jema na kila mmoja ana kila sababu ya kusifia jambo hili,"alisema Masiroli.

Akizungumza katika mkutano huo,Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo alisema aliguswa na taarifa ya kuezuliwa kwa shule hiyo akiwa katika vikao vya Bunge na kuamua kuaga ili kuweza kushiriki moja kwa moja katika tatizo hilo.

"Ndugu zangu niliguswa na suala hili na kuamua kuaga bungeni lakini kabla sijafika hapa tayari niliagiza mafundi kuja kuangalia athari iliyopatikana hapa na kuanza kwa ujenzi,lakini kazi hii inapaswa kushikiana na kila mwana Rorya na mdau wa elimu ili vijana wetu waendelee kusoma.

"Sasa hivi suala la elimu ndio linaloangaliwa katika kila sehemu,lazima majengo haya yakamilike na watoto wetu wasome naomba kila mmoja aje kuchangia ili madarasa haya yaliyoezuliwa yaweze kukamilika,"alisema Lameck.

Katika harambee hiyo ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vilivyoezuliwa na upepo iliyoongozwa na Mbunge huyo zaidi ya shilingi milioni mbili zilipatikana zikiwemo ahadi ya mifuko 19 ya saruji.


Post a Comment