Ndugu
wanahabari, kwanza kabisa napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wangu, ili niweze
kuzungumza na watanzania kupitia kwenu kuhusu hatari kubwa inayolikumba taifa
ya madawa ya kulevya.
§ Biashara
haramu ya dawa za kulevya imekua kwa kasi sana hapa nchini miaka ya hivi
karibuni licha ya kuwa na vyombo lukuki vya ulinzi na usalama na licha ya kuwa
na Tume maalumu ya kudhibiti madawa ya kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
§ Kwa
mujibu wa Taarifa ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera Uratibu na Bunge Mhe. Wiliam Lukuvi tarehe 26
Juni, 2013 siku ya maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya huko
Dodoma ni kwamba katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012 watuhumiwa 10,799
walikamatwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini.
Aidha, watanzania wapatao 240 walikamatwa na madawa ya kulevya katika nchi za
Brazil, Pakistan na Afrika ya kusini na hivyo kutia doa taswira ya Tanzania
katika jumuiya ya kimataifa. Kutokana na kukithiri kwa biashara hii haramu,
Serikali kupitia maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita madawa ya kulevya
duniani ilitangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya kuwa ni janga la taifa.
§ Mtakumbuka
pia kwamba hivi majuzi, muda mfupi baada ya Serikali kutangaza kuwa
biashara ya dawa za kulevya ni janga la taifa , walikamatwa wasichana wawili ambao
ni watanzania huko Afrika ya kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya
yenye thamani ya zaidi ya randi milioni 42.6 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 6 za kitanzania.
§ Ndugu
wanahabari, matukio yote haya yametokea ndani ya kipindi cha miaka sita tu ya
utawala wa Serikali ya awamu ya nne ambapo kuna viongozi wa juu Serikalini
ambao waliwahi kusema kuwa wanawajua watu wanaojishughulisha na biashara haramu
ya dawa za kulevya lakini mpaka sasa hawajawataja wahusika na wala hakuna hatua
yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.
§ Ndugu
wana habari, miongoni mwa viongozi wa
serikali na taasisi nyingine waliosema kuwa wanawafahamu wafanya biashara
ya madawa ya kulevya ni:-
i.
Rais Jakaya Kikwete, ambaye alipiga hatua
kubwa zaidi na kusema anawajua hata viongozi wa dini wanaofanya biashara hiyo.
Licha ya maaskofu na viongozi wengine wa dini kumtaka Rais awataje wahusika hao
wa madawa ya kulevya ili kuuweka ukweli
wazi, Rais hajafanya hivyo mpaka sasa.
ii.
Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya: huyu alisema anayo majina ya vigogo (kwa maana ya viongozi)
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini hajaweka majina hayo
hadharani na wala haijulikani kama wahusika hao wamechukuliwa hatua yoyote hadi
sasa.
iii.
Mbunge wa Mwibara – Kange Lugola alisema katika
bunge la bajeti 2013/2014 kuwa kama Rais na Kamishna wa tume ya kudhibiti dawa
za kulevya wanawajua “kwa majina” watu wanaojihusisha na biashara za dawa za
kulevya na hawataki kuwataja watu hao wala kuwachulia hatu yamkini watu hao ni
miongoni mwa mawaziri ndio maana kuna kigugumizi cha kuwataja na kuwachukulia
hatua. Tangu Mhe. Kange Lugola alihusishe baraza la Mawaziri na kashfa hiyo ya
kuhusika na biashara ya dawa za kulevya hakuna hatua yoyote ilivyochuliwa na
Serikali kuthibitisha au kubatilisha kauli hiyo.
iv.
Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Bw. Reginald
Mengi aliwahi kutoa taarifa ya wazi kuwa
kuna kundi la matajiri wanaoshirikiana na viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwa
wanapanga njama za kumwekea mtoto wake dawa za kulevya ili wambambikizie kesi ya
dawa za kulevya na hivyo kuchafua heshima ya Bw. Mengi na familia yake. Ndugu
mengi alisisitiza katika taarifa yake kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano kwa
jeshi la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika ili kubaini njama hizo na
kuchukua hatua stahiki kwa wahusika lakini mpaka leo Ndugu Mengi hakuhojiwa ili
kuthibitisha kauli yake jambo linaloashiria kwamba kuna ukweli katika kauli
yake.
Baada ya matukio yote haya na baada ya
Serikali kukaa kimya kuhusu matukio hayo, mimi kama Waziri Kivuli wa Mambo ya
Ndani ya Nchi na kwa niaba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ninatoa tamko kama ifuatavyo:
1. Rais
Jakaya Mrisho Kikwete awataje na kuwachukulia hatua watu aliosema anawafahamu
wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya la sivyo akubali kubeba shutuma
kwamba Serikali yake ndio Mratibu Mkuu wa biashara ya dawa za kulevya ndio
maana anashindwa kuchukua hatua.
2. Kamishana
wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma
juu ya hatua alizochukua dhidi ya
wahusika wa biashara ya dawa za kulevya aloiosema anawafahamu la sivyo, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuwashawishi wananchi kuamini kwamba yamkini na yeye yumo katika mtandao wa
wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya ndio maana anasita kuwachukulia
hatua wahusika hao ambao alishakiri kuwa anawafahamu.
3. Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa
ni tatizo gani linaloikabili mamlaka yake hadi kufanya viwanja vya ndege vya
Tanzania kuwa ndio njia rahisi ya kuingiza na
kusafirishia madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki?
4. Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi wawajibike kwa
kutoa maelezo kwa umma kuwa ni kazi ipi
wanayofanya ikiwa madawa ya kulevya yanaingizwa nchini na kusafirishwa nje ya nchi kwa kasi kubwa
zaidi?
HITIMISHO: Ni
vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao
ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za
kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa
na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea
kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu
taifa na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na
kusimamia usitawi wa wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba
kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa
dalili kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.
MUHIMU:
IKIWA SERIKALI ITAENDELEA KUPUUZIA JAMBO HILI AMBALO LINALIANGAMIZA TAIFA, BASI
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI ITAENDESHA OPERESHENI NCHI NZIMA ILI WANANCHI WAPIGE KURA KWA WAHUSIKA WAKUU
WA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA, NA BAADA YA ZOEZI HILO, TUTAANIKA HADHARANI
(KWA KUWATAJA MAJINA) WAHUSIKA WA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA.
______________________________________
Vincent
Josephat Nyerere (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI
BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA MABO YA NDANI YA
NCHI
Post a Comment
0 comments