1

DIWANI wa Kata ya Tai iliyopo Wilaya ya Rorya kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na Mwenyekiti wa Chama hicho wilayani hapa, Cristopher Masirori amenusurika kushambuliwa na Wananchi wenye hasira kali baada ya kukamatwa ugoni na mwanamke wa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo.

Akizungumza na BLOG HII,mume wa Mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Thobias Rujora maarufu kwa jina la Ninja mkazi wa kijji cha Kiariko,alisema usiku wa saa 2 julai 23 alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akimuuliza kama ndiye anayeitwa Thobias na kumueleza mke wake yupo kwenye mazingira ya hatari na afike mara moja maeneo ya Obwere Shirati.

Alisema mtu aliyempa taarifa alisema mke wake ameingia katika nyumba ya kulala wageni na kiongozi mmoja wa Chama cha siasa na kuamua kuzifatilia habari hizo kwa kuwachukua baadhi ya jamaa zake hadi Obwere Shirati katika nyumba hiyo ya kulala wageni aliyetajiwa kuwa inaitwa Treepo A.

Rujora alisema baada ya kufika katika nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa kolidoni aliamua kupiga simu ya mke wake na kusikia ikiita na kuamua kutoka nje na kupiga simu kituo cha polisi Shirati kwa ajili ya kuomba msaada wa polisi ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

"Baada ya kuona simu ya mke wangu ikiita chumbani watu niliamua kutoa taarifa polisi lakini watu niliowaacha pale nje walitaka kutumia nguvu ya kuvunja mlango na kuwazuia maana walikuwa na hasira na na jambo baya lingetokea nami nlijipa ujasiri juu ya tukio hilo,"alisema Rujora.

"Niliwazuia na wakanielewa na baada ya muda mfupi askari polisi wapatao sita kutoka kituo cha polisi Shirati walifika na kuingia ndani na kugonga mlango zaidi ya mara sita ndipo ulipo funguliwa na Diwani huyo kukutwa ndani na mke wangu wakakamatwa.

Alipooulizwa kama katika siku za nyuma aliwahi kupata taarifa juu ya kuwepo kwa taarifa zozote za uhusiano kati ya kiongozi huyo na mke wake,Rujora alisema hajawahi kupata taarifa na kudai Diwani huyo amekuwa akilalamikiwa kwa vitendo vya kuwa na mazoea mabaya na wake za watu.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kituo cha polisi Wilaya ya kipolisi Shirati Musa Msenya alisema walizipata taarifa hizo kwa mtu anayedaiwa kuwa mume wa mwanamke aliyekamatwa na Diwani hayo na kuamua kwenda katika eneo la tukio..

"Ni kweli tukio hilo lilitokea Obwere Shirati nasi kuchukua uamuzi wa haraka kufika eneo la tukio baada ya kupata taarifa tayari watu walitaka kujichukulia sheria mikononi na tuligonga mlango baada ya muda kadhaa tulifunguliwa na wale wanaodaiwa kushikwa ugoni kuamua kuondoka nao.

"Tusingefika eneo lile mapema jambo baya lingeweza kutokea maana tuliwakuta wananchi wakiwa na hasira huku wakiwa wameshika siraha za jadi na kutoa maneno yaliyoathiri kutaka kumdhuru Mwenyekiti huyo wa Chadema Rorya,"alisema Msenye.

Wakizungumza na BLOG baadhi ya Wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema Diwani huyo amekuwa na tabia ya kuwa na mahusiano na wake za watu na katika siku za hivi karibuni alifikishwa polisi na baadae ofisi za Ustawi wa Jamii akilalamikiwa na mkazi wa Rorya kuchukua mke wake ambaye aliacha watoto.


Post a Comment