0
WAKULIMA wa zao la pamba mkoa Mara wamewalalamikia wataalamu wa zao hilo kwa kushindwa kusimamia majukumu yao na kupelekea mkulima kuendelea kuwa masikini huku watu wachache wenye viwanda wakiendelea kutajirika kwa kutumia nguvu zao.

Wamedai takwimu zinazofanywa na wataalamu kuhusu zao hilo na usimamizi wa ununuzi sio sahihi hivyo kufanya fedha nyingi za wakulima wanazostahili kuzipata kutowafikia baadwa ya uzalishaji wa zao la pamba unaotokana na nguvu zao.

Hayo yalisemwa kwenye kikao cha pili cha wadau wa sekta ndogo ya pamba kilichofanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji wa mkoa wa Mara kilivhowashilikisha wakulima wa zao hilo,wakuu wa Wilaya,wataalamu  na wadau mbalimbali wa zao hilo.

Mmoja wa wakulima hao kutoka Wilayani Serengeti Renald Reuben alisema wataalamu wanapaswa kuwa karibu na wakulima katika msimu wa pamba kuanzia maandalizi,upandaji hadi kwenye msimu wa mavuno ili kuweza kudhibiti ubadhilifu wakati wa utolewaji wa pembejeo na uununuzi wa pamba.

Alisema moja ya sehemu ambayo wakulima wanapata adha kubwa na kunyonywa ni kwenye mizani inayotumika wakati wa ununuzi wa pamba kupitia kwa mawakala ambao wamekuwa wakifanya wizi kwa kuvuruga mizani hivyo kupelekea mapato mengi ya wakulima kupotea huku mkulima akiendelea kuwa masikini.

Reuben alisema licha ya Serikali kutilia mkazo kilimo cha pamba bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wakulima wa zao hilo na kudai bila kutatuliwa kwa dhati wataendelea kuwa watu duni huku wachache wakinufaika.

Akizungumza katika kikao hicho,Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pmaba Tanzania Gabriel Mwala alisema ili kuhakikisha wakulima wa zao la pamba wananufaika na kilimo hicho,bodi itahakikisha inatoa leseni kwa wanunuzi wanaomjali mkulima kwa kufanya uwekezaji kwa ajili ya kilimo kwa mfumo wa kilimo cha mkataba ili kumuondolea adha mkulima.

Alisema kampuni ya ununuzi na uchambuzi wa pamba itakayopewa leseni ni ile itakayotoa fedha kwanza ajili ya maandalizi ya kilimo cha pamba na kuthibitishwa na wakuu wa Wilaya kwa kampuni hiyo kushiriki katika shughuli za maendeleo katika Wilaya ambayo wamepanga kwenda kununua pamba wakati wa msimu ili kumpa unafuu mkulima.

Akifunga kikao hicho kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikao Mkuu wa mkoa wa Mara John Tupa,Mkuu wa Wilaya ya Butiama Angelina Mabula alisema pamoja na mambo mengine ili kumuinua mkulima wa zao la pamba lazima mfumo wa ununuzi wa pamba ufanywe na vikundi vya wakulima wenyewe ili kuepukana na mawakala wasio waaminifu na wadanganyifu katika mizani na kkupitisha azimio la kusajiliwa kwa vikundi hivyo kabla ya msimu mpya.

Mabula alisema ni muhimu bodi ya pamba kuhakikisha mfumo mpya wa kuandaa mikataba ya wakulima na wanunuzi inawashirikisha wanasheria na kuwataka wakulima kufuata kanuni bora za kilimo ili kuwa ni tija na kuzingatia mbegu bora zinazohitajika
 
 

Post a Comment