0
 
Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Rorya John Adiema,amefunguliwa mashitaka na mke wake ambapo pamoja na mambo mengine Mwanamke huyo ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mara kutengua ndoa yao na kupewa talaka.
 
 Kesi hiyo ambayo  ni ya kwanza kutokea Nchini kwa Kanisa hilo kuhusu Askofu kufikishwa Mahakamani imepangwa kusikilizwa novemba kumi na nane mwaka huu katika Mahakama hiyo mjini Musoma.
 
Mke huyo wa Kiongozi Mkuu wa kanisa la Angilikana Jimbo la Rorya Peres Adiema,akizungumza baada ya kufungua shauri hilo Mahakamani hapo,alisema pamoja na talaka pia anamdai mume wake huyo haki zake za msingi walizochuma wakiwa kama wana ndoa.
 
Mama huyo alidai amefikia uamuzi wa kudai talaka baada ya kuishi katika manyanyaso kwa muda wa miaka 12 sasa bila kujua hatima ya manyanyaso hayo ni lini,hivyo amefungua kesi ya madai namba moja katika mahakama ya mkoa na kupangwa kuanza kusikilizwa novemba 18 mwaka huu.
 
Alisema chanzo cha yeye kudai talaka yake Mahakamani ni hatua iliyochukuliwa na mume wake ambae ni Askofu ya kumtaka aache kazi ili waweze kuendelea kuishi pamoja ili hali awali kabla hajaolewa na baada ya kuolewa alikuwa ni muuguzi katika hosptali ya Misheni ya Kowaki Rorya inayomilikiwa na kanisa la Romani Katoliki.
 
Alidai baada ya kufunga ndoa na Askofu huyo ambaye hapo awali alikuwa Mchungaji katika Kanisa la Anglikana Musoma alitafuta uhamisho wa kutoka Rorya ili aweze kufanya kazi akiwa karibu na mumewe,ambapo hakufanikiwa kupata tena kazi ya Uuguzi.
 
Peres alisema  baada ya kuishi na mumwe kwa muda wa mwaka mmoja  wa ndoa mume huyo alianza kumtaka aache kazi ili waweze kuendelea kuishi pamoja la sivyo atoke kwake,jambo ambalo alidai lilimsumbua sana akili,hivyo akaamua kuacha kazi na kukaa nyumbani.
 
Alida baada ya kukaa nyumbani mume huyo alikuwa akimfanyia manyanyaso ambayo hakutarajia kuyapata kutoka kwa mtu mwenye hadhi aliyokuwa nayo mumewe kama mchungaji,hivyo alichukua uamuzi wa kutafuta tena ajira upya ili aweze kuondokana na manyanyaso madogo madogo.
 
Alisema alifanikiwa kupata ajira katika Hospitali ya Mkoa ambapo hata hivyo mumewe aliendelea kumsumbua hadi kwa mwajiri wake kwa kuweka shinikizo la kumwachisha kazi hali amabayo alidai ilikuwa ikimpa wakati mgumu katika utendaji kazi.
 
“Ilifikia hatua akanifukuza kwake,akaniambia nichague….kama nataka kazi  niishi na kazi kama nataka ndoa niache kazi ili niiweze kuishi nae,nami nikaona ni msalaba ni bora nikaishi mwenyewe maisha yangu”alidai mama huyo huku akibubujikwa na machozi.  
 
Peres alidai mwaka 2012 alichukua uamuzi wa kuondoka,ambapo Askofu huyo alikatalia watoto  wawili aliozaa naye,mkubwa akiwa na umri  wa miaka tisa na mdogo akiwa na miaka saba huku akimyima ruhusa ya kuonana na watoto hao.
 
“Nilizaa na Askofu watoto wawili ambao niliwaacha,lakini hata hao watoto nikisia ni wanaumwa kiasi gani sina ruhusa ya kuwaona na hata hataki kuniona nikiwa  nyumbani kwake ndio maana nimeomba talaka na mahakama itoe uamuzi ambao itaona unafaa”alisema Peres.
 
Kiongozi mmoja wa dini wa kanisa hilo ambaye  aliomba kutotajwa gazetini,alisema sheria za kanisa hilo zinasema endapo kiongozi wa juu (Askofu) akifikishwa Mahakamani kwa kosa kama hilo anapaswa kujihudhulu nafasi hiyo au kufukuzwa ndani ya kanisa.
 
“Sheria ziko wazi, sasa kama askofu anafikishwa Mahakamani kwa kosa la unyanyasaji na kushindwa kuimudu familia yake sasa itakuwaje kwa kondoo anaowaongoza…hivyo kufikishwa mahakamini tu kwa madai kama hayo kunamuondolea hadhi yake ya kuwa kiongozi wa kanisa”alisema.
 

Post a Comment