0
 
WANANCHI wanaoishi kandokando ya Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara, wanahitaji msaada wa haraka wa chakula kutokana na uvamizi wa mashamba na maghala ya kuhifadhia chakula uliofanywa na tembo kutoka hifadhi hiyo walio wavamia.
 
Katibu wa Kamati ya madiwani wa Chama cha Mapinduzi wilayani Serengeti Richard Nyakera, alikiambia kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwa Wananchi waishio katika kata nane za Halmashauri hiyo wanakabiliwa na njaa.
 
Nyakera alizitaja Kata ambazo uvamizi huo wa makundi ya tembo umesababisha upungufu wa chakula ni Kata za Sedeco, Manchira, Kyamba, Nyansurura, Machochwe, Natta, Isenye na Ikoma na kudai kama jitihada za haraka hazitafanywa na Serikali huenda vikatokea vifo vya Wananchi kutokana na njaa.
 
Alisema pamoja na kuomba msaada huo wa chakula kamati hiyo ilisema kwa vile Serikali inafanya doria kupambana na majangili basi  pia ifanye kila juhudi kuhakikisha kuwa tembo hao wanarudishwa hifadhini na kuwatoa katika maeneo ya Wananchi ambao wanatishia maisha yao pamoja na kuharibu chakula.
 
Katibu huyo wa madiwani wa CCM ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sedeco alisema Serikali wilayani humo inatakiwa kutangaza tatizo la upungufu wa chakula wilayani humo  sasa ni janga hivyo kuhitaji hatua za haraka kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Manchira Michael Shaweshi (CCM) alisema suala la uvamizi wa tembo katika makazi ya Wananchi na kuharibu mashamba pamoja na chakula ambacho tayari kimehifadhiwa kwenye maghala sio la kulikalia kimya na Serikali kupitia Wizara ya Mali Asili na Utalii wanapaswa kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na hali hiyo.

Alisema makundi ya tembo kwa sasa yamekuwa yakiingia hadi katika maeneo ambayo awali walikuwa hawafiki jambo ambalo linatishia zaidi mazao ya wakulima pamoja na maisha yao na kudai kwa sasa tayari tembo hao wameshaharibu mashamba mengi ya Wananchi na  kuwaacha wakikabiliwa na njaa.

Shaweshi alisema kutokana na hali hiyo kuna kila sababu kwa Halimashauri ya Wilaya ya Serengeti kutangaza baa la njaa kutokana na uhalibifu mkubwa ambao umefanywa na tembo ambao walitoka hifadhini na kuvamiwa mashamba ya Wananchi na kuharibu mazao.

Katika kikao hicho cha Baraza la madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halimashauri hiyo ya Serengeti kiliandaa Sheria ndogondogo zilizotungwa chini ya kifungu cha 168 juu ya taratibu za Ufugaji,Ulinzi na Usalama,Afya ya Jamii,Elimu,Ushiriki katika shughuli za Maendeleo na kilimo za Halimashauri ya Kijiji ili kuondokana na matatizo mbalimbali ya wagugaji na Hifadhi ya Serengeti pamoja na masuala ya Wananchi.
 

Post a Comment