0
 
 
MTU mmoja aliyedaiwa kuhusika na wizi wa mihogo kwenye shamba la mkulima ameuwawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa,kukatwakatwa na mapanga kisha kuchomwa moto baada ya kudaiwa kuiba mihogo.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari,kamanda wa polisi mkoani Mara Ferdinand Mtui alisema tukio la kuuwawa kwa mtu huyo lilitokea januari 6 majira ya saa 11 alfajiri katika kijiji cha Mkirira Kata ya Nyegina Wilaya ya Butiama akiwa ndani ya shamba akipakia mihogo kwnye gunia.
 
Kamanda Mtui amemtaja mtu aliyeuwawa amefahamika kwa jina la Akuku Aringo (47)ambaye ni mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda mkazi wa Nyakato Manispaa ya Musoma.
 
Alisema Wananchi waliojichukulia sheria mikononi kabla ya kumchoma moto mtu huyo walianza kumpiga mapanga kichwani,kuvunjwa mikono na miguu yote kasha kumchoma moto na kufa hapo hapo.
 
Katika tukio lingine kamanda wa polisi mkoani Mara alisema mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mashaka Lazaro (48)mkazi wa Kijiji cha Ligamba wilayani Bunda ameuwawa kwa kuliwa na mamba wakati akivua samaki kwenye mto Rubana
 
Alisema tukio hilo lilitokea januari 4 majira ya saa 4 usiku maeneo ya Tamau Kata ya Kuzugu Tarafa ya Serengeti wilayani Bunda na kupelekea kifo cha mtu huyo ambaye alidaiwa kupiga kelele baada ya kukamatwa na mamba.
 
Kufuatia matukio hayo,Kamanda Mtui ameendelea kusisitiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua na kuacha tabia za kujichukulia sheria mikononi.
 
Aidha mkuu huyo wa polisi mkoani Mara aliwataka wananchi kuwa waangalifu kwenye maeneo wanayofanyia shughuli za uvuvi na mito ili kuepuka kushambuliwa na kuliwa na mamba

Post a Comment