Mkurugenzi
wa Kituo cha Matangazo ya Televisheni cha Afrika (Africa TV) Bwana
Muharami Iddiss akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi Cheti maalum cha Africa TV cha kuitumia ZBC – TV kurusha
Vipindi vyake.
Makamu
wa Pilio wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja
na uongozi wa Africa TV ulioambatana na baadhi ya Viongozi wa Taasisi za
Dini mara baada ya mazungumzo yao yalioyofanyika Ofisini kwake Vuga
Mjini Zanzibar. Kulia
ya Balozi Seif ni Mkurugenzi wa Africa TV Bwana Muharami Idriss na
Kushoto yake ni Mshauri wa Africa TV Zanzibar Bwana Kassim Haidar
Jabir.
*********************************************
Uongozi
wa Kituo cha Matangazo ya Televisheni cha Afrika { Africa TV } wenye
Makao Makuu yake Nchini Sudan umenasihiwa kuendelea kufanya kazi zake
za kuelimisha jamii hasa umma wa Kiislamu kwa kuheshimu maadili ya kazi
zao ili kufanikisha vyema majukumu yake katika utaratibu uliojipangia.
Nasaha
hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na
Uongozi wa Afrika TV ulioambatana na baadhi ya Viongozi wa Taasisi za
Dini ya Kiislamu ambao upo Zanzibar kujitambulisha rasmi ukijiandaa na
utaratibu wa kutangazwa matangazo yake kupitia Shirika la Utangazaji
Zanzibar { ZBC - TV }.
Balozi
Seif alisema Vituo vya Habari kama Afrika TV inayotoa matangazo ya
Dini vinaweza kusaidia kwa asilimia kubwa kuelimisha Jamii mfumo mzuri
wa kufuatwa katika kulinda Mila, Maadili na Taratibu za Kidini jambo
ambalo husaidia kuiepusha jamii kujiingiza katika matendo maovu.
Alisema
wapo baadhi ya masheikh na Walimu wa Dini hutumia fursa wanazozipata
ndani ya vyombo vya Habari kwa kupotosha umma kujiingiza katika vitendo
viovu ambavyo husababisha kutetereka kwa amani na utulivu wa Nchi.
Aliusisitiza
Uongozi huo wa Afrika TV kuwa makini na wahadhiri wanaowatumia kwenye
vipindi vyao ambao wakati mwengine hutia ushawishi unaoleta uchochezi
na hatimae kukosekana kwa utulivu wa jamii.
“
Tuwe na uhakika kwamba kinachotolewa na Afrika TV kinaelimisha vyema
umma na kuwepuka ushawishi ambao unaweza kuleta fadhaa na kukosekana kwa
utulivu wa moyo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
“
Tunategemea sana kwamba Programu za Afrika TV zinatuelimisha vya
kutosha na kupata faida iliyokusudiwa ya kueneza Daawa “. Alisisitiza
Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo kupitia Shirika la Utangazaji { ZBC TV } kwa
kushirikiana na Vituo vyengine mbali mbali vya Matangazo vya kimataifa
katika dhana na kuipatia Jamii Taaluma, Habari pamoja na kuipatia Elimu.
Mapema
Mkurugenzi wa Afrika TV Bwana Muharami Idriss alisema fikra za
kuanzishwa kwa Afrika TV iliibuka mnamo mwaka 2010 baada ya ufinyu wa
kukosekana kwa vyombo vya Habari vinavyopaswa kuelimisha Umma wa
Kiislamu ndani ya Bara la Afrika.
Bwana
Muharami alisema Afrika TV ilianza rasmi matangazo yake mwaka 2011 kwa
kutumia Lugha Tano na kuongeza Lugha ya Kiswahili mwaka 2012 na baadaye
lugha Tatu mwaka 2013.
Alieleza
kwamba Uongozi wa Kituo hicho ulikuwa na azma ya kufungua Tawi la
Studio yake hapa Zanzibar ili kuziongezea nguvu zaidi zile za Dar es
salaam na Mombasa Nchini Kenya ikiwapa fursa zaidi ya kutoa Taaluma
wahadhiri na Walimu wa hapa Zanzania.
Akitoa
shukrani zake kwa Uongozi wa Kituo hicho cha Afrika TV Naibu Katibu wa
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Nauman Jongo alisisitiza umuhimu wa
kufuatwa kwa taratibu za vyombo vya Habari ili kuepuka mapema cheche za
ushawishi zinazoweza kuleta mfarakano ndani ya jamii hapo baadaye.
Sheikh
Jongo alisema baadhi ya vyombo vya Habari nchini vilipata fursa ya
kutoa matangazo yake lakini vikajikuta whadhiri wake wakitumia zaidi
ushawishi ulioonekana kuleta mgongano wa kimawazo ndani ya mafundisho
ya dini.
Lengo
la Kituo cha Matangazo cha Afrika TV ni kutoa Matangazo yake kwa zaidi
ya lugha 10 katika kipindi kifupi kijacho zitakazotoa huduma ya
Taaluma katika mataifa mbali mbali Barani Afrika.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikutana na Mhariri Muandamizi wa Gazeti la Financial Report { F.T. }
lenye Makao Makuu yake London Nchini Uingereza Bwana Rohit Devan Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika
mazungunzo yao Bwana Rohit Devan anayesimamia miradi maalum kwenye
Gazeti hilo ndani ya Kanda ya Afrika alisema Uongozi wa Gazeti hilo
umeamua kuitangaza zaidi Zanzibar katika Nyanja za Kiutamaduni,
Uwekezaji na Utalii.
Bwana
Rohit Devan lisema wahadhiri, Wahariri na hata vyombo vingi vya Habari
vya Kimataifa zimekuwa vikiitangaza Zanzibar hasa zaidi katika eneo la
Kisiasa na Kihistoria.
“
Ukifanya utafiti wa haraka haraka unakuta waandishi wengi wa Kimataifa
wameitangaza sana Zanzibar katika nyaja ya Kisiasa wakati Visiwa hivi
vina rasilmali nyingi za Uwekezaji hasa katika sekta ya Utalii, biashara
na Utamaduni “. Alifafanua Bwana Rohit Devan.
Mhariri
huyo muandamizi wa Gazeti ya Financial Report alielezea matumaini yake
kwamba kwa kupitia Gazeti hilo Zanzibar itajiuza vyema Kimataifa kwa
vile limekuwa likichapishwa kwenye machapisho manne kila siku katika
vituo vya Miji ya Paris, London, Washington na Monako.
Naye
kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliupongeza Uongozi wa Gazeti hilo kwa uwamuzi wake wa kutaka
kuitangaza Zanzibar Kimataifa katika Nyanja za Uwekezaj.
Balozi
Seif alisema hatua hiyo itaipa Zanzibar muelekeo mzuri wa kufahamika
zaidi katika Nyanja za Kimataifa katika suala la uwekezaji ambapo tayari
Sekta ya Utalii imeshapewa msukumo zaidi katika kuongeza nguvu za
Uchumi wa Zanzibar.
Aliuomba
Uongozi wa Gazeti hilo la Financia Report kuwa huru katika kuwasiliana
na Taasisi na makampuni ya uwekezaji yaliyopo Nchini ili yapate fursa
ya kujitangaza kupitia Gazeti hilo la Kimataifa.
KWA HISANI YA SUFIANIMAFOTOBLOG
Post a Comment
0 comments