MFANYABIASHARA MARTINI KOROGO AKICHANGIA KWENYE MGOMO WA WAFANYABIASHARA
MKUU WA WA MKOA WQA MARA JOHN TUPA KUSHOTO AKITETA JAMBO NA MENEJA WA TRA BAADA YTA MGOMO WA WAFANYABIASHARA
SEHEMU YA MADUKA YALIYOFUNGWA MJINI MUSOMA
WAFANYABIASHARA wa mjini Musoma wamegoma kufungua biashara
zao katika maduka ya huduma mbalimbali wakidai kutokuelewa mfumo wa matumizi ya
mashine za kieletroniki EFDs pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato(TRA)kuwapa majibu yasiyo
mazuri na kugoma kupokea vitabu vyao vya mauzo kwa ajili ya mahesabu hali
iliyopelekea mkuu wa mkoa wa Mara pamoja na meneja wa TRA kukutana nao.
Katika mgomo huo ambao uliitikiwa na wafanyabiashara wote
mjini hapa,walidai TRA wameshindwa kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara
kutokana na matumizi ya mashine hizo na kinachoonekana kwa sasa kuna mpango
ambao unakusudiwa na watumishi wa TRA kuwabana zaidi baada ya kugoma kupokea
vitabu vyao vya mauzo kwa ajili ya kukadiliwa kodi.
Katibu wa wafanyabiashara wadogo mjini Musoma Bugoro Marwa
alisema wameanza kuona mapema manyanyaso kutoka kwa baadhi ya watumishi wa TRA
kwa kushindwa kupokea vitabu vyao hivyo wameamua kuweka mgomo wa kutokufungua
maduka ili wapewe muongozo mzuri na wafanye biashara zao kwa amani.
Alisema baadhi ya
wafanyabiashara walikwenda katika ofisi za TRA lakini walikutana na manyanyaso
kutoka kwa watumishi wake na kuona ni vyema kuchukua maamuzi ya kugoma kufungua
biashara zao ili waweze kupata ufumbuzi juu ya kile ambacho kimeanza kuonekana
baada ya kugoma kupokelewa vitabu vyao vya mahesabu.
Bugoro alisema hakuna mfanyabiashara ambaye anaweza kugomea
kulipa kodi kwa kuwa hakuna Serikali inayoweza kuendeshwa bila kodi lakini
mfumo unaofanywa wa ukusanyaji kodi sio rafiki kwa wafanyabiashara na unazidi
kuwarudisha nyuma.
Alisema licha ya kuhusiana na suala la mashine za EFDs katika mji wa Musoma
kumekuwa hakuna mahusiano mazuri kati ya watumishi wa TRA na wafanyabiashara
katika ukusanyaji wa kodi hali iliyopelekea wafanyabiasha wengi kuhama Musoma na
kwenda kufanya biashara katika miji mingine na kuuacha mji wa Musoma ukiwa na
maendeleo duni.
“Hapa lazima tuelezane ukweli,wafanyabiashara wengi wa mji
wa Musoma wamehama na kwenda miji mingine kutokana na manyanyaso ambayo
wamekuwa wakifanyiwa na watumishi wa TRA na kufanya mji huu ukiwa nyuma
kimaendeleo kila kukicha,”alisema
Bugoro.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina la
Beatrece Libamba alisema wakina wanawake wajasiliamali ndio wanaoumizwa sana na
mfumo wa ukusanyaji kodi wa TRA kutokana na kuchukua mikopo katika taasisi za
fedha na kupelekea kushindwa kurejesha kutokana na makusanyo ya kodi kutoka
TRA.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato(TRA) mkoa wa Mara Joseph Karinga
alisema bado wanaendelea kupokea vitabu vya wafanyabiashara kwa hesabu za mwezi
januari na kama kuna mtumishi ambaye aligoma kupokea vitabu wampelekee ofisi
kwake ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa.
Akizungumza na wafanyabiashara hao baada ya kukutana nao
kutokana na mgomo huo.mkuu wa mkoa wa Mara John Tupa alisema ni vyema
wafanyabiashara kabla ya kuchukua uamuzi wa kugoma wangemuona na kukaa pamoja
ili kuweza kuzungumza na kuona kero zinazowakabili kutoka kwa watumishi wa TRA.
Alisema ni vyema kama kuna suala lolote linalo wakwanza
wafanyabiashara ofisi yake ipo wazi na yupo tayari kukutana nao na kama
itaonekana mtumishi yoyote ambaye afuati maadili ya kazi atachukuliwa hatua na
mtu yoyote asisite kutoa taarifa kwenye vyombo vinavyohusika.
Tupa alisema kutokana na nafasi yake ya mkuu wa mkoa hawezi
kuzungumzia suala la mashine za EFDs kwa kuwa tayari limeshazungumzwa na
Seriksali inalo hivyo anaamini linafanyiwa kazi na kudai suala la kufanya mgomo
linawaathiri wengi na kusema yupo tayari kukutana nao ili kuweka meza ya
mazungumzo na kuyafikisha mahala husika.
Kufuatia hali hiyo baadhi ya wananchi wa mji wa Musoma
wameiomba Serikali kuangalia suala la wafanyabiashara na mashine za EFDs kwa
kuwa mgomo wa wafanyabiashara unakwamisha huduma mbalimbali ikiwemo hata maduka
ya dawa kufungwa kutokana na mgomo huo.
Walisema kila mahala hapa nchini wafanyabiashara wamekuwa
wakilalamikia mashine hizo na kuiomba Serikali kutazama upya suala hilo kwa
kuwa wanaoathirika ni pamoja na wananchi ambao wamekuwa wakishindwa kupata
huduma kutokana na mgomo wa wafanyabiashara unaojitokeza mara kwa mara.
Post a Comment
0 comments