0Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ usiku wa leo itafanya onyesho maalum ya kusherekea siku ya wapendanao ‘Valentine Day’, kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. 

Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka amesema kuwa pia bendi hiyo itatumia onyesho hilo kumtambulisha mpiga  tumba wao mpya ambaye atamrithi MCD aliyefariki dunia hivi karibuni.

Asha amesema bendi hiyo itamkaribisha tena mpiga besi wao Jojo Jumanne aliyerejea kutoka bendi ya Ruvu Stars.

Mkurugenzi huyo amesema watatumia onyesho hilo kutambulisha nyimbo zao mpya na baadhi ya vyombo vipya.

“Tunaomba watu wajitokeze kwa wingi waje waangalie onyesho letu  maalum  kwani hili siyo  la kukosa. Kumbuka Valentine Day hufanyika mara moja kwa mwaka,” alisema Asha.

Naye mratibu wa onyesho hilo Joseph Kapinga amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika kilichobaki ni muda kufika ili mashabiki wapate uhondo.

Onyesho hilo limeandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts kwa hisani ya Dodoma Wine, Freditto Entertainment na Saluti5.

Mratibu huyo amesema kuwa siku hiyo Twanga Pepeta pia itapiga nyimbo zao za zamani zilizowapatia umaarufu.

Baadhi ya nyimbo hizo ni Kisa Cha Mpemba, Fainali Uzeeni, Mtu Pesa, Safari 2005, Aminata, Busu  2000 na nyinginezo.

Bendi hiyo inayotamba kwa staili ya Kisigino pia itapiga nyimbo zao za kisasa kama Nyumbani ni Nyumbani, Dunia Daraja,‘Mwana Dar es Salaam’, ‘Shida ni Darasa’, ‘Rafiki Adui’, ‘Mwisho wa Ubaya ni Aibu’, ‘Nazi Haivunji Jiwe’ na ‘Sitaki Tena’. 

Bendi hiyo inaundwa na wanamuziki kama Kalala Junior, Dogo Rama, Saleh Kupaza, Luiza Mbutu, Badi Bakule, Greyson Semsekwa, Rama Pentagon, Mirinda Nyeusi, Kala Junior, na Janet Isinika katika safu ya uimbaji.

 Kwa upande wa upigaji vyombo wapo James  Kibosho, Moshi Kinanda, Miraji Shakashia, Gody Kanuti, Philipo Paulo a.k.a. Kaposho, huku safu ya unenguaji ikiwa, Saidi Matongee, Mandela, Abdilayi Zingu,  Sabrina Pazi, Vicky, Hamida na Grace.

Post a Comment