0
 
 
Imeandikwa na Josefly Muhozi
Moja kati ya matukio makubwa yaliyoteka ‘attention’ ya watu wengi ni picha na video zilizowekwa kwenye ukurasa wa Facebook na boss wa Mtanashati Entertainment, Ostaz Juma zikimuonesha mwimbaji toka Mwanza PNC akiwa amepiga magoti na kuonesha ishara ya mikono kama anaomba mbele ya boss huyo aliyetulia kwenye kochi akiwa amekunja 4.

Picha na video hizo ziliwekwa na Ostaz Juma mwenyewe kwenye ukurasa wake wa Facebook na kuandika, ““hahaha jamani mziki ni kazi pnc arudi kuomba msamaha ili aendelee kufanya kazi mtanashati.”

Haikuchukua muda, watu mbalimbali ambao ni wadau wa muziki wa kizazi kipya walipaza sauti wakilaani kitendo hicho kupitia mitandao ya kijamii wakiwemo wasanii mbalimbali ambao hawakusita kumchana Ostaz kwa kile kilichoonekana kuwa ni kumdhalilisha mwimbaji huyo.

Lakini wapo mashabiki ambao waliporomosha matusi kufuatia tukio hilo na habari hiyo kusambaa kwa nguvu kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyompelekea Ostaz kudai kuwa siye aliyeziweka picha hizo. Lakini kilichowashitua wengi baadae, ni pale ilipoonekana post nyingine kwenye ukurasa wake akiwaponda watangazaji wa Tanzania na wasanii kuwa wanasumbuliwa na njaa.

“Naona watu mmeguswa sana na mimi kuanika picha ya PNC katika mitandao et, tatizo wasanii wa Tanzania mnanjaa sana kuanzia watangazaji Radio na wasanii njaa ndizo zinazo wasumbua...”

Lakini baadae aliongea na Moko Biashara aka One B wa Times Fm kueleza kuwa ukurasa wake metekwa na wezi wa akaunti za watu mtandaoni (hackers) na kwamba hiyo sio post yake.

“Daah, nshachanganyikiwa rafiki yangu watu wamehack akaunti yangu wanaandika matusi wanatukana watu..hadi hapa mimi nimeshachanganyikiwa hadi hata kuongea siwezi bro.” Alisema Ostaz.

Nadhubutu kusema kwa msisitizo kuwa picha hizo ziliwekwa na Ostaz Juma kwa jinsi nilivyozifanyia utafiti na kuzingatia kauli yake aloyoniambia kwa mara ya kwanza, “Ndio PNC kunipigia magoti na kuniomba radhi, lakini sasa mimi nikaamua kuwaonesha watanzania kwamba PNC amerudi kweli kuniomba msamaha. Je, kama kweli PNC alikuwa analalamika ‘Ostaz anafanya kazi zake hanijali hanisaidii…”


Hata hivyo sina uhakika…huenda kweli hakuandika kauli ya kuwaponda watangazaji na wasanii…nasema huenda kwa kuwa muda mchache baada ya kudai kuwa akaunti yake ilikuwa imetekwa na hackers na kubadili ‘password’, aliingia tena na kuifuta post hiyo na kuandika nyingine ya kuomba radhi na kueleza kuwa ilikuwa imetekwa kwa kipindi kile. Kwa upande wangu ‘no comment’ kwenye hilo.

Anyways, kwa maelezo yote hapo juu bila shaka umepata picha nzima ya tukio hilo japo kwa ufupi.
 
Sasa niende moja kwa moja kwenye mada na lengo langu, mkasa huu unapaswa kuwa zaidi ya somo la kawada kwa Ostaz Juma na wengine hasa watu maarufu ambao huichukulia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Instagram n.k kama sehemu fulani tu ya kuandika unachotaka kama jinsi ulivyopewa uhuru ‘What’s on your mind’. Kumbe unatakiwa kufikiria sana kabla hujaandika na sio kuandika tu kile kilichoko kichwani kwako, kama unajali.

Ntatumia fikra ambazo nadhani alikuwa nazo Ostaz Juma kabla hajayaona matokeo ya alichokifanyana, matokeo yaliyomchanganya.

Huenda Ostaz Juma alikuwa bado anafikiria kuwa Radio, Television na magazeti pekee ndio vyombo vya habari vikubwa kuliko ‘social media’, wazo ambalo ni la kizamani kwa dunia ya sasa hivi.

Huenda Ostaz alikuwa hafahamu kuwa hivi sasa kwa kiasi kikubwa Traditional Media kama Radio, Television na magazeti zimeungana na ‘New Media’ ambazo ni mitandao ya kijamii, tovuti pamoja na blogs na habari husambaa kwa nguvu kupitia vyombo hivyo huku vikibadilishana.  

Habari nyingi zina-break kwenye mitandao bila kujali muda na huzua mijadala mikubwa kama hiyo.

Huenda alikuwa hafahamu kama, unachoandika Facebook kikishachukuliwa na watu wakaanza kushare hata ukifuta bado kitaendelea na kufika mbali zaidi na hata watu kuhamishia kwenye magroup ambayo huwa na maelfu ya watu au hata kuhamishiwa ‘watsapp’ na huenda wakati unajitetea watu hao wasisikie ama wakakupuuza.

Huenda yeye aliona ana marafiki 2,258 akaona sio watu wengi na kwamba isingekuwa issue serious kiivo kama ambavyo angesema kwenye radio na vituo vya television.  

Huenda alikuwa hafahamu kama picha inaongea lugha zote duniani (universal language) hata bila kufuatilia nani kaandika nini. Hata mchina atakuwa ameielewa picha hiyo kwa lugha yake!

Ngoja nimfungue macho kama kweli alikuwa anafikra hizo.
Hadi kufikia mwishoni mwaka jana, takwimu zilionesha kuwa watu zaidi ya billioni 1.2 duniani kote wanatumia Facebook na kwamba hao ni active members, na kwa wastani kila mtumiaji ana marafiki zaidi ya 130 ambao anaweza ku-share nao habari na ikasambaa duniani kote kwa muda mfupi.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 ya watu wazima wanaingia kwenye mitandao mbalimbali ambapo hata kama hawajajiunga na mitandao ya kijamii wanatembelea tovuti mbalimbali ambazo zinachukua habari kwenye mitandao ya kijamii.
Habari kama hizo zinazotokea Facebook huendelea kusambaa pia kwenye mitandao mingine ya kijamii kama Instagram, na hata Twitter ambayo inachukua 18% ya watumiaji wote wa mitandao, ambao wengi wao ni ‘active users’ na ndio kundi kubwa la watu wenye ushawishi (influential) kama watu maarufu. Twitter ina watumiaji zaidi ya milioni 640.

Kwa upande wa Instagram, kwa mfano Diamond akiishare picha hiyo wataiona watu zaidi ya 90,000 ambao wanaweza pia kushare, na huenda watu wakaiamini moja kwa moja habari hiyo kuwa kuwa msanii wanaempenda kalaani kitendo hicho.

Kwa takwimu hizo, ni vyema kufahamu kuwa kupitia mitandao ya kijamii hususani watu ambao wanafanya biashara inayotokana na kuuza kazi zilizobebwa na ‘image’ yao kama vile kazi za muziki, wanaweza kutengeneza biashara kubwa kwa kuwa wateja wengi wanaoweza kufanya maamuzi wako kule.

Uamuzi wa kuandika kitu kwenye mitandao ya kijamii kwa watu wenye biashara kama hiyo nikitolea mfano wa Ostaz Juma lazima uwe unamnyima uhuru wa kuandika kila anachofikiria tu, bali kuwaza mara mbili ama tatu matokeo ya kuweka mtandaoni kile anachofikiria.

Mtu kama Ostaz ambaye anawasaidia wasanii wa Tanzania, anatakiwa kufahamu kuwa msaada wake kwa wanamuziki hao kwao ni biashara ambayo inahitaji zaidi ya pesa kwa kuwa wanauza vitu viwili ambavyo ni muziki na ‘image’. Uropokaji wa mambo unaweza kuvunja image ambayo kuijenga itamgharimu msanii huyo zaidi ya pesa alizopewa kurekodi wimbo, kushuti video, kupigishwa pamba na hata pesa ya promotion.

Kwa mtu maarufu anayetegemea kuuza kutokana na sapoti ya watu, anatakiwa kufahamu kuwa ukurasa wake wa Facebook sio kijiwe cha washikaji zake ambacho anaweza kusema chochote kilicho kichwani kwake bila kujali na wakakipotezea baadae.

Ingawa Radio, Television na magazeti inawafikia watu wengi zaidi duniani na ina nguvu, ni vyema kwa mtu kama Ostaz na wengine wenye nafasi katika jamii kuelewa kuwa kila chombo cha habari kina nguvu kubwa na sio vyema kukilinganisha na chombo kingine ama kukipuuza.

Yale yalitokea sebuleni kwake (Ostaz Juma) yalipaswa kuwa faragha kwao wote wawili na sio kuyaweka kwenye mitandao ya kijamii.

Mwisho, ni vyema kwa mtu yeyote kutumia kanuni ya mitandao ya kijamii kuwa usiandike kitu chochote kwenye mtandao wa kijamii ukiwa na hasira ama ukiwa ‘too emotional’. Jitahidi kuvumilia kukaa nacho moyoni kwa muda na baada ya kutafakari unaweza kushare na watu.

Post a Comment