MBUNGE
wa jimbo la Tarime ametumia kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili
ya kugharimia vitabu katika shule mbalimbali za Sekondari katika
jimbo hilo,lengo likiwa ni kuinua kiwango cha elimu na kufanya wilaya
hiyo kuwa na amani na kuwa kimbilio la watu katika Nyanja mbalimbali
za kiuchumi.
Akizungumza
na waandishi wa habari,mbunge huyo Nyambari chacha
Nyangwine,alisema kuwa baada ya kuingia madarakani mwaka 2010
alikumbana na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya elimu
hatua ambayo ilimfanya kuchukua hatua za haraka za kuchangia
vitabu hivyo katika shule za Sekondari ikiwa ni sehemu ya kutatua
changamoto hizo.
Alisema
kuwa wakati anachaguliwa kuwa mbunge wa Tarime, wilaya hiyo
ilikuwa inatakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa amani ya
kudumu huku akiwa na shule 18 za sekondari lakini kwa juhudi
zake,madiwani na halmashauri wameweza kujenga shule hadi kufikia
38 sasa hatua ambayo imefanya wilaya ya Tarime kupata mabadiliko
makubwa kimaendeleo.
“Wakati
nachaguliwa kulikuwa na shule 18 za sekondari na zikiwa na
changamoto kubwa nikaamua kuanza na tatizo la vitabu vya kujifunzia
na kufundishia na hadi sasa nimechangia vitabu vya zaidi ya
bilioni moja huku tukiwa tumejenga shule za sekondari 20 kutoka 18
zilizokuwepo”alisema na kuongeza.
“Watu
wanashangaa kuona Tarime leo ni wilaya inayokalika kwa kuwa na
amani ya kudumu huku ikipaa kimaendeleo,mafanikio yote haya
yametokana na elimu”aliongeza mbunge huyo.
Alisema
kuwa amani hiyo ya kudumu kwa kiasi kikubwa pia imechangiwa na
juhudi zake za kukemea baadhi ya watu waliotaka kuongoza
wilaya hiyo kwa kuwagawa wazee wa mila ili waweze kupata nafasi
za kisiasa kwa kutumia koo watokazo.
“Tena
wanasiasa hao “uchwara” wakiwemo kutoka katika chama changu
wanakwenda kushawishi wazee wakisema mimi sitagombea tena ubunge
mwaka kesho,sasa nawaambia nitagombea na nitashinda kupita wakati
ule,wasivuruge amani kwa kutaka kuchaguliwa”alisema na kuongeza.
“Tarime
ilikuwa ni wilaya ya mfano wa mapigano ya koo nchini,wakina
mama,vijana walipoteza maisha,watu walishindwa kufanya shughuli
za uzalishaji mali kama kilimo,kuzikana,kutembelea hata kufikia hatua
ya kubaguana kutokana tu na uchu wa madaraka uliofanya baadhi ya
wazee wa mila kutumika vibaya kwa kusaidia wanasiasa…hali hii
ilinitisha sana na nikasema wakati ule wa sherehe ya kuwashukuru
wapiga kura kuwa ningependa niongoze Tarime moja na leo ninyi
mnashuhudia Tarime ni moja”alisema.
Hata
hivyo alisema baadhi ya wanasiasa hadi sasa hawapendi hali
hiyo,wamekuwa wakitumia pesa kuwashawishi hata baadhi ya viongozi
wa mila kuungwa mkono kwa kutumia koo zao kitu ambacho alisema
kinaweza kuvuruga amani iliyopo na kutosaidia kabisa maendeleo ya
wananchi wa Tarime.
Alisema
hivi sasa ameanza kusimamia ujenzi wa chuo cha ufundi VETA kwa
ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana wanahitimu elimu ya darasa la saba
na kumaliza kidato cha nne wanajiunga na mafunzo ya ufundi ili
kuwawezesha kujiajiri wenyewe katika kukabiliana na tatizo kubwa la
ajira kwa vijana.
Mbunge
huyo wa jimbo la Tarime,ametumia nafasi hiyo kuutaka uongozi wa mgodi
wa North Mara kutekeleza mara moja ahadi zake kwa vijiji vinavyozunguka
mgodi huo ikiwa ni pamoja na kulipa fidia ya ardhi katika maeneo hayo
ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikisababisha kuteteleka kwa amani
katika eneo hilo.
“Niliwahi
kutoa kauli ya kufanya maandamano ya kuwatoa wawekezaji hao kwa
kutumia nguvu ya umma ili kushinikiza mgodi kutekeleza ahadi
zake,tulisitisha baada ya kutueleza kuwa wangetekeleza ahadi hizo
na ulipaji wa fidia lakini hadi sasa hawajatekeleza”alisema
Nyangwine.
Kwa
sababu hiyo aliutaka uongozi wa mgodi huo kutekeleza ahadi hizo kabla
ya mwezi desemba la sivyo atalazimika kutumia nguvu ya umma kushinikiza
malipo hayo hata kama nguvu hiyo inaweza kusababisha maafa katika
eneo hilo ili kuwatendea haki wananchi hao ambao alisema pamoja na
kuzungukwa na madini lakini wamekuwa wakiishi katika timbwi kubwa la
umasikini.
Mbunge
Nyangwine aliongeza kwa kuitaka serikali kuwatendea haki wananchi
wanaozunguka migodi za dhahabu ili waweze kunufaika na rasimali
hizo badala ya kuwaona wananchi hao kama wahalifu huku
wakiwakumbatia wawekezaji pekee hatua ambayo alisema imekuwa
ikichangia migogoro mingi katika maeneo hayo.
Post a Comment
0 comments