FAZEL JANJA
Musoma.
MOJA ya malengo ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais
Dk. John Pombe Magufuli, ni kupambana na rushwa ambayo ni adui wa haki na
kikwazo kikubwa cha maendeleo.
Hata wakati akilifungua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mjini Dodoma Novemba 20, 2015; kwa kuonesha msisitizo juu ya dhamira
yake hiyo, Rais alitoa ahadi ya kuanzisha Mahakama Maalumu ya kushughulika na makosa ya Rushwa na Ufisadi.
“Katika kushughulikia tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama
ya rushwa na ufisadi, ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili
havitanikwamisha…” ilisema sehemu ya hotuba ya Dk. Magufuli.
Katika hotuba yake hiyo rais anaoneshwa kukerwa na vitendo
vya rushwa na ufisadi vilivyoshamiri nchini na kwamba vinawanyima haki wananchi
na kuitia serikali hasara ya mabilioni ya fedha; huku akifafanua kuwa fedha
hizo zinazopotea kwa njia ya rushwa zingeweza kutumika kugharamia miradi mbalimbali
ya maendeleo.
Magufuli anakwenda mbali na kunukuu maneno ya Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Nyerere aliyoyatoa Mei, 1960 wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya
Muungano. “Rushwa haina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini
wakati wa amani, rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Rais anasisitiza kuwa hayo ni maneno makali ya mtu na kiongozi
aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi; anasema
kauli hiyo ya Mwalimu inatahadharisha hatma ya taifa letu endapo tutaendelea
kuendekeza rushwa na ufisadi.
Aidha katika hotuba yake hiyo rais anatanabaisha wazi kuwa
chuki ya wananchi kwa sasa ni dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi na kwamba ni
dhahiri kuwa wamechoka kabisa na hawako tayari (tena) kuendelea kuivumilia
serikali itakayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Ndiyo maana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU)
mkoani Mara, kwa kuitikia na kuzingatia agizo hilo la Rais Dk. John Pombe
Magufuli la kutomuangusha katika kutimiza malengo yake hayo; imepanga mikakati
madhubuti kuhakikisha inakwenda sambamba na kasi ya serikali yake chini ya
kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Akizungumza hivi karibuni na vyombo vya habari mkoani hapa,
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara Holle Makungu anataja sehemu ya mikakati hiyo
sambamba na taarifa ya miezi mitatu (Januari – Machi, 2016) ya utekelezaji wa
majukumu ya taasisi hiyo.
Anasema mikakati na majukumu hayo ni kwa mujibu wa Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 na sheria zinazohusiana,
kama ile ya kuzuia utakatishaji fedha namba 12 ya 2006 na ile ya mali
zinazopatikana kwa njia za kihalifu (the Proceed of Crime Act, Cap 256) ya 1991.
Makungu anaitaja mikakati hiyo pamoja na mambo mengine; kuwa ni
kuhakikisha kwamba watumishi wote wa umma wanaotumia vibaya nyadhifa zao kwa vitendo vya rushwa na ufisadi,
wanachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kupitia waajiri
wao na kufikishwa mahakamani mara moja.
Mbinu nyingine ni kufuatilia fedha za umma kwenye
halimashauri kama zinafanya kazi stahiki na iliyokusudiwa; kuendelea kutoa
elimu kwa madiwani, wakuu wa idara na wananchi kwa ujumla juu ya namna
mbalimbali za kuzuia na kupambana na rushwa ikiwa ni pamoja na kuvishauri vyama
vya siasa kuwanyang’anya kadi wabunge ama madiwani wanaotumia vibaya nyadhifa
za kisiasa, kama kinga kwao dhidi ya tuhuma za makosa ya rushwa na ufisadi.
Aidha Makungu anafafanua kuwa ofisi yake imekuwa ikitekeleza
majukumu yake ya kila siku kupitia utaratibu wa aina tatu ambao ni pamoja na kufanya
uchunguzi, kutoa elimu kwa umma sanjari na udhibiti.
Katika kipindi cha miezi mitatu dawati la elimu kwa umma limeimarisha
kwa njia ya elimu Klabu za Wapinga Rushwa 55 ndani ya mkoa, ili kuwaandaa
vijana na wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, ambapo semina 31 zimefanyika;
mikutano ya hadhara 13 ikiwa ni pamoja na kuchapisha vijalida, Makala, maonesho
na vipindi kadhaa vya redio na machapisho mengine 2,888 yenye ujumbe mbalimbali
wa vita dhidi ya rushwa yaliyowafikia watu zaidi ya 11,000.
Aidha kwa upande wa udhibiti Makungu anasema katika maeneo
mbalimbali walikofanya udhibiti, dhibiti 7 zimefanyika katika Idara ya Afya,
Elimu, Maji na Ardhi.
Akizungumzia kwa upande wa ukaguzi wa miradi mbalimbali, mkuu
huyo wa Takukuru anasema kuwa kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu, wamekagua
miradi zaidi ya 20 ya maendeleo iliyokuwa ikiendelea na iliyokamilika hapa
mkoani; wakifuatilia kwa makini kabisa thamani ya pesa kulinganisha na ubora wa
viwango vya utekelezaji wa mradi husika (value for money).
Anasema ni kupitia utaratibu huo pamoja na mambo mengine,
wamebaini kuwa miradi mingi imekuwa ikifunguliwa kila mwaka kupitia mbio za
mwenge lakini kwa sababu ya rushwa, mingi kati yake ama imeshindwa kukamilika
kabisa, ama imekamilika katika viwango duni licha ya kuwepo kwa wataalamu na
washauri wa kitaalamu katika halimashauri zetu.
“Tumebaini baadhi ya makandarasi kulipwa fedha zote hata
kabla ya mradi kukamilika…mfano ujenzi wa nyumba za walimu Shule ya Sekondari
Kyabakari, fedha zote 125,000,000/= zimekwishalipwa kwa mkandarasi wakati jiko
katika moja ya nyumba hizo haijakamilika…tunamtaka kandarasi kukamilisha kazi
hiyo ndani ya mwezi mmoja la sivyo sheria ichukue mkondo wake.” Anasema Makungu.
Mkuu huyo wa Takukuru mkoani Mara anasema ndiyo sababu ofisi
yake katika kipindi cha miezi mitatu tu imepokea taarifa/malalamiko 179 kutoka
vyanzo mbalimbali ambapo kati yake 150 yamefunguliwa majalada ya uchunguzi wa
awali, 7 yamefanyiwa udhibiti, moja limehamishiwa idara nyingine huku
walalamikaji 21 wakipewa ushauri wa kisheria.
Aidha anasema malalamiko hayo yaliyopokelewa mengi yanahusu
miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya TASAF III pamoja na mishahara
hewa (wahusika wakiwa ni Tamisemi), ambapo malalamiko mengine yanahusu mahakama,
Jeshi la Polisi, NHIF, TRA, TFDA, Uhamiaji, Afya (hospitali ya mkoa na
zahanati), Muwasa na Tanesco.
“Hadi sasa kesi 42 zinaendelea katika mahakama mbalimbali za wilaya
na mkoa wa Mara huku kesi tano zikiwa tayari zimekwishatolewa hukumu kwa mujibu
wa sheria za nchi.” Anasema Makungu.
Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa Makala hii kuhusiana na
madai kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiwakamata watuhumiwa ‘vidagaa’ wa rushwa na
kuwagwaya ‘mapapa’ Makungu anakanusha vikali madai hayo.
“mimi natekeleza majukumu yangu katika ngazi ya mkoa…sijui ni
vigogo gani hao unaotaka niwakamate…nimemfikisha mahakamani Katibu Tawala wa
Mkoa (RAS), DED wa Serengeti na hata Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Musoma…kigogo gani mwingine unayemtaka?” Anahoji.
Makungu anawataka wananchi wote kushirikiana na Takukuru kwa
kutoa taarifa sahihi na kwa wakati juu ya jambo lolote lenye harufu ya rushwa
na kwamba Sheria ya Takukuru Na. 51 na 52 inamlinda mtoa taarifa.
0655 872873, 0784 872873.
Post a Comment
0 comments