0
 KUFUATIA vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga kutokea wakati wa kujifungua,daktari bingwa wa kichina wa mama na watoto,Li Qiang,ametoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara ili kupunguza na kumaliza vifo hivyo.

Akizungumza wakati wa kutoa mada ya uzazi salama,daktari huyo amesema wakati wa kujifungua wapo akina mama ambao wanatoa damu nyingi na hivyo kupelekea vifo hivyo hivyo ni muhimu kupeana ujuzi zaidi namna ya kuepusha vifo hivyo.

Amesema zipo hatua ambazo zikichukuliwa wakati mama anapokuwa akijifungua kuna uwezekano mkubwa wa kumuokoa mama mjamzito pamoja na kichanga na kudai ni muhimu kukumbushana.

Li Qiang amesema tatizo la kutokwa na damu nyingi kwa mama mjamzito ni chanzo cha kwanza cha kupoteza maisha hivyo lazima njia na elimu mbalimbali zikawa zinatolewa ili kupunguza au kumaliza kabisa vifo hivyo kwa mama wajawazito.

Amesema katika elimu ambayo ameitoa hasa kwa madaktari na wauguzi wanao wahudumia mama wajawazito kwa asilimia kubwa itawasaidia pale wanapokuwa wana wahudumia na kuwafanya kujifungua wakiwa salama.

"Mwezi huu nimeshuhudia kifo cha mama mjamzito kutokana na kuvuja kwa damu nyingi na nimeona nikutane na watoa huduma ili tuweze kushirikiana kuhakikisha vifo hivi vinapungua na kuvimaliza kabisa kwa njia ya utaalamu,"alisema Dk.Li Qiang.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara,Godfrey Elias,amesema mkakati wa hospitali hiyo ni kuhakikisha ina punguza kwa asilimia kubwa vifo hivyo au kumaliza kabisa kwa kutoa elimu mblimbali.

Amesema licha ya mikakati hiyo kwa hospitali wananchi pia wanaombwa kujitokeza kuwa wanachangia damu ili kuweza kushirikina kwa pamoja kuweza kumaliza vifo hivyo.

Elias amesema katika kipindi hiki cha wiki ya uchangiaji wa damu na kipindi kingine ni muhimu kila mmoja akaguswa na kuamua kujitokeza kuchangia damu ambapo itasaidia pamoja na kuokoa vifo vya mama wajawazito kutokana na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua.

Post a Comment