0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Musoma mkoani Mara, imewahukumu kwenda jela miaka 30 watu wawili baada ya kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha (kisu) na kupora fedha na simu moja ya mkononi aina Techno.

Waliohukumiwa kutumikia kifungo hicho jela sambamba na kulipa fidia  ya sh laki mbili na kuchapwa viboko 24 kila mmoja ni  Paulo Aloyce na Nyamuhanga Musa ambao ni wakazi wa kata za Nyakato na Rwamlimi katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Wakati akisoma hukumu hiyo, hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Richard Maganga, alikumbushia shitaka lililokuwa likiwakabli na kusema kwamba mnamo January 24 mwaka huu majira ya saaa 3 asubuhi, mlalamikaji katika kesi hiyo Ndera Nyaki, mkazi wa Musoma Mjini akiwa maeneo ya kiwanda cha nguo cha Musoma(MUTEX) akielekea kanisani alivamiwa na watuumiwa na kumtishia kwa kisu kabla ya kupora vitu hivyo.

Katika kutekeleza dhamira yao walimpekua mlalamikaji mifukoni na kupora fedha taslimu sh 11,000 pamoja na simu moja aina ya techno vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi laki moja.

Mahakama ilielezwa kuwa, watuhumiwa katika harakati ya kukimbia mlalamikaji alipiga yowe na kufanikiwa kuwatia mbaroni.


Watuhumiwa walifikishwa polisi na kufunguliwa jalada la unyang’anyi wa kutumia silaha kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo upande wa mashitaka ulileta mashahidi watano akiwemo mlalamikaji huku kwa upande wa watuhumiwa walijitetea wenyewe katika kesi hiyo.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Maganga, alisema Mahakama imeridhika na ushadi uliotolewa na upande wa mashitaka hivyo watuhumiwa hao kutiwa hatiani baada ya kubainika walitenda kosa hilo kinyume cha Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai Na 16 ya mwaka 2002 sura ya 29 kifungu  cha 286 na 287.

Katika Hukumu hiyo,Hakimu wa kesi hiyo alitoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kila mmoja pamoja inayoendana na viboko 24 akidai makosa ya unyang'anyi yamekithili katika Manispaa ya Musoma na adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine.

Awali licha ya washitakiwa hao kupewa nafasi ya kujitetea, bado utetezi wao haukuwa na sababu za msingi za kuishawishi ,Mahakama hiyo iwapunguzie adhabu na ilikubaliana na hoja ya upande wa  mashitaka ulioongozwa na Wakili wa serikali,Theophili Mazuge, wa kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa watu wengine katika jamii.

Post a Comment