0

SERIKALI mkoani Mara imesema itatumia nguvu zote katika kuwalinda wawekezaji hasa wazawa katika sekta ya madini ili uwekezaji huo uweze  kutatua tatizo kubwa la ajira kwa vijana na kuchangia pato la taifa.
Mkuu wa mkoa wa Mara,Magesa Mulongo,ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha Kataryo baada ya kutembelea na kukagua hatua za awali za uzalishaji katika mgodi wa kati wa dhahabu wa Cata Mine uliopo halimashauri ya Musoma na Butiama ambao unamilikiwa kwa ubia wa Mtanzania na raia mmoja wa nchini Canada.

Amesema sekta ya madini kwenye migodi ni moja ya eneo ambalo linatoa ajira nyingi hususani kwa vijana hivyo hakuna budi wawekezaji wanaowekeza kwenye sekta hiyo kuangaliwa na kupewa ushirikiano na serikali ili waweze kufanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Mulongo ambaye alikuwa kwenye moja ya ziara zake za kuangalia shughuli za kiuchumi zilizopo mkoani Mara,amesema wapo watu ambao kazi yao ni kuleta fitina baina ya wawekezaji na wananchi na kuibua migogoro ambayo haina tija na hata kufikia kukimbiza wawekezaji kwa kufunga shughuli zao.

Akitolea mfano wawekezaji waliokuwa wamewekeza eneo la Buhemba kwaajili ya uchimbaji na kuondoka na kuacha eneo hilo likiwa halina shughuli zozote kutokana na fitina mbalimbali na kudai hawezi kuona wawekezaji wakishindwa kulindwa na kusumbuliwa kutokana na fitina.

"Serikali ya mkoa wa Mara haita sita kuwalinda wawekezaji pale wanapokuwa wanafuata sheria na kuzingatia taratibu zote na kuona baadhi ya watu wanaanzisha chokochoko kwa kuwa watu hawa wanasaidia vijana wetu ajira na kuongeza pato la taifa.

"Ukiangalia pale Tarime wanaweza kuwa wanajisifu kutokana na kipato kwenye halimashauri yao lakini wanabebwa na mgodi wa Acacia uliopo kule kutokana na gawio wanalopata hivyo mkuu wa wilaya nakuomba sana uwaangalie wawekezaji hawa wasisumbuliwe,"amesema Mulongo.

Akitoa taarifa za shughuli za mgodi huo ambao ni wa kwanza kumilikiwa kwa sehemu kubwa na watanzania,afisa mahusiano wa mgodi huo,Alnazir Mawji,amesema hivi sasa mgodi huo umeanza kufanya majaribio ya uzalishaji huku akiwaomba wananchi kuwaunga mkono ili kuwezesha mgodi kuchangia pato la taifa na shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake mkurugenzi mzawa wa mgodi huo,Mahuza Nyakirang'anyi,amesema hadi sasa kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji rasmi tayari wameshachangia shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa barabara,madaraja na uchimbaji wa visima vya maji na kuwaondolea hadha wananchi.

 Hata hivyo baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji vinavyozunguka mgodi huo licha ya kupongeza mchango mkubwa ambao tayari umetolewa na mgodi huo katika kusaidia miradi ya maendeleo wameomba vijana wanaotoka kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi kupewa kipaumbele cha ajira ili kuwawezesha kiuchumi.
 Mkurugenzi mzawa wa mgodi,Mauza Nyakirang'anyi(kushoto)akimuangalizia kufia ngumu mkuu wa mkoa wa Mara,Magesa Mulongo,kabla hajaanza kutembelea mgodi huo akiwa na viongozi mbalimbali"TAZAMA PICHA ZA MATEMBEZI HAYO"


















Post a Comment