0

MBUNGE wa Jimbo la Bunda mjini,Ester Bulaya(Chadema) ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza inayokaa mjini Musoma chini ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga,Noel Chocha,anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015 kuwa alishinda kihalali kwenye uchaguzi huo.

Katika utetezi wake mara baada ya kula kiapo mahakamani hapo chenye aya 11 kilichosomwa na Wakili wake,Tundu Lissu,amesema alitangazwa kama Mbunge wa Jimbo la Bunda mjini na mjibu maombi wa 2 ambaye ni msimamizi wa uchaguzi mara baada ya taratibu zote ikiwemo zoezi la uhesabuji wa kura kukamilika.
 
Amesema wakati wa kuhesabu kura na kutangazwa kwa matokeo na msimamizi wa uchaguzi,mawakala wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo walikuwepo na walishiriki hatua zote hadi ulipofika wakati wa kutangazwa kushinda ubunge wa Jimbo la Bunda mjini

Baada ya utetezi wa Ester Bulaya kutolewa Mahakamani,marumbano ya kisheria baina ya mawakili wa upande wa waleta maombi na wajibu maombi uliibuka na kudumu kwa zaidi ya saa 3 ambapo majibishano ya vifungu vya kisheria yakitawala.

Majibizano hayo yalianza mara baada ya wakili wa waleta maombi,Costantine Mutalemwa,kuiomba Mahakama kuondoa aya 7 kati ya 11 zilizokuwa kwenye utetezi wa Ester Bulaya,kwa kile alichokieleza havimo kwenye utaratibu wa awali uliowasilishwa Mahakamani.

Katika aya ya 7 ya utetezi wa Ester Bulaya,inayodai kasoro ya kura 164794 zilizotangazwa awali na msimamizi wa uchaguzi badala ya kura 69369 za wapiga kura halali hazikuathiri matokeo ni moja ya aya zilizopingwa na wakili Mutalemwa Mahakamani hapo.

Wakili Mutalemwa alisema masuala ambayo yameibuka kwenye utetezi wa Ester Bulaya ni mapya na suala la idadi ya wapiga kura ni moja ya kipengele ambacho wateja wake wanaopinga matokeo hayo waliwasilisha Mahakamani.
 
"Naomba Mheshimiwa Jaji aya ya 2,3,4,5,6,7 na 8 ziondolewe kwenye utetezi wa Ester Bulaya na kubakiza aya ya 1,9,10 na 11 kwa kuwa haya nnazoomba ziondolewe ni mpya na hazipo kwenye utaratibu wa awali na aya 4 pekee sina pingaamizi nazo",alisema Mutalemwa.

Kufuata maombi ya wakili Mutalemwa,Wakili anayemtetea Mbunge wa Jimbo la Bunda mjini,Ester Bulaya,Tundu Lissu,alisema baada ya kusikiliza pingamizi dhidi ya kiapo cha shahidi ameikumbuka kauli ya aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Mahakama ya Afrika Mashariki,Sir.Charz Nyubon,ya kuwataka mawakili kuacha kuweka mapingamizi yasiyo na msingi.

Alisema kitendo cha mawakili kuweka mapingamizi yasiyo na msingi ni kupoteza muda wa Mahakama kwa mujibu wa kauli ya Rais huyo na kumuomba Jaji anayesikiliza kesi hiyo kuendelea na ushahidi wa mtoa ushahidi kwa kuwa muda wa kupoteza kwenye ushahidi haupo.

Lissu alisema Amri ya 19 kifungu cha 3 (1) hakijasema kuwa na uthibitisho kwenye viapo kama ambavyo anadai wakili Mutalemwa kwenye maombi yake ya kutaka kuondoa baadhi ya aya za utetezi wa mteja wake.

Kwa upande wake Wakili wa serikali,Angela Lushagamba,alisema hana pingamizi lolote kwenye kiapo cha utetezi wa, Ester Bulaya,uliotolewa mahakamani hapo na kuiomba Mahakama kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi.

Akitoa maamuzi juu ya hoja zilizoibuka Mahakamani hapo,Jaji Noel Chocha,alisema anaona dalili za kusikilizwa kwa muda mrefu wa shauri hilo kutokana na hoja mpya ambazo ziliibuka Mahakamani.

"Kuna vitu vipya ambavyo vimeibuka kwa siku ya leo na kunahitajika nipate muda wa zaidi ya saa 5 kuweza kuvifanyia kazi na kusikiliza haya yote yanayotolewa na mawakili ni katika pia kuja kuyafanyia kazi katika sheria hizi za kesi za uchaguzi hivyo naomba nihailishe shauri hili hadi kesho(leo)saa 7 mchana.

Post a Comment