0
 

 MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza inayosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wa Jimbo la Bunda mjini imeyatupilia mbali mapingamizi 7 aliyowekewa Mbunge wa Jimbo la Bunda mjini, Ester Bulaya, kwenye kiapo chake cha ushahidi na wakili wa waleta maombi wa kesi hiyo, Costantine Mutalemwa.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya anayesikiliza kesi hiyo,Noel Chocha,alitumia saa 2 kuweza kutoa ufafanuzi wa vifungu vya sheria na hoja mbalimbali ambazo zilimshawishi kuamua kuzikubali aya hizo ziendelee kuwemo kwenye kiapo cha shahidi na kubaki kama kumbukumbu muhimu kwenye kesi hiyo.

Alisema Amri ya 19 ya kanuni ya 3(1) ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ambayo ilitumiwa na wakili Mutalemwa anayewatetea waleta maombi haina maana kusomwa pekee yake na kutumiwa kuweza kuziondoa aya hizo.

Jaji huyo alisema anakubaliana na hoja ya wakili, Tundu Lissu,anayemtetea mjibu maombi ikiwemo Amri ya 23 ya Tangazo la Serikali namba 447 la mwaka 2010 ambalo linamtaka mjibu maombi kusema kitu chochote hata kama hakukitaja kwenye maelezo yake ya awali.

"Fungu la 4 hadi la 8 halimuhusu mjibu maombi kama ilivyoweka na wakili wa waleta maombi kuwa ni mambo mapya yaliyoletwa Mahakamani na mimi katika hili na kutokana na na amri ya 23 sioni jambo jipya lililoletwa hivyo pingamizi lolote haliwezi kukubaliwa.

"Kwa maoni yangu ni muhimu kufanya maboresho katika masuala kadhaa ya mashauri ya uchaguzi hili kesi hizi zinapokuwa zinasikilizwa ziweze kumalizika kwa mapema zaidi,"alisema Jaji huyo.

Baada ya maamuzi ya Jaji huyo kutoa Mahakamani hapo,Wakili anayewatetea waaleta maombi wa kesi hiyo,Costantine Mutalemwa,alimuomba Jaji kuhailisha kesi hiyo hadi oktoba 17 kutokana na mawakili wote kukubaliana hoja ambayo kisha kuhailishwa na Jaji na kumtaka mjibu maombi wa kwanza,Ester Bulaya kujiandaa kuanza kutoa ushahidi wake.

Nje ya Mahakama hiyo Mutalemwa alisema baada ya maamuzi ya Jaji yaliyotolewa Mahakamani sasa wanajiandaa kuanza kumuuliza maswali shahidi wa upande wa wajibu maombi kama ilivyoamuliwa na Jaji.

Alisema kukataliwa kwa mapingamizi 7 waliyokuwa wameyaweka kati ya 11 kwa mjibu maombi wa kwanza ni maamuzi ya jaji na kilichobaki ni kijipanga kwaajili ya hatua nyingine ya mwenendo wa kesi hiyo

Kwa upande wake wakili anayemtetea mjibu maombi wa kwanza,Tundu Lissu,alisema maamuzi ya Jaji ni hatua nzuri kwa kuwa katika kiapo hicho cha shahidi kuna masuala ya msingi ambayo katika ushahidi wa waleta maombi walikana Mahakamani.

Alisema katika ushahidi wa Wasira na wenzake walikana kwamba wakati wa kuhesabu kura hawakuwepo kwenye chumba ya kuhesabu kura lakini kwenye kiapo kilichopokelewa Mahakamani na Jaji shahidi ameeleza namna ambavyo walishiriki kikamilifu katika hatua zote za uhesabuji wa kura na kutangazwa kwa matokeo.

"Tunaishukuru Mahakama Kuu imezipokea hoja zetu za kupinga kuwekwa kwa mapingamizi 7 kwa shahidi na kuamua kuyatupilia mbali na hii ni sehemu ya ushindi kwakuwa mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa ni mengi na wakili wa waleta maombi.

"Jumatatu shahidi ataanza kutoa ushahidi wake na ntamuongoza vizuri katika kutoa ushahidi wake ili kuweza kuweka kumbukumbu nzuri  ya zaidi katika kesi hii ya uchaguzi inayoendelea Mahakamni hapa,"alisema Lissu.















Post a Comment