0
 AFISA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) anayefanya kazi kwenye kituo cha ushuru na forodha cha mpaka wa Sirari wilayani Tarime,jina tunalo,anatafutwa na vyombo vya dola akituhumiwa kukwepesha ushuru halali wa serikali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Tarime ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo,Glorius Luoga,amesema taarifa za kukwepeshwa kwa kodi halali zilitolewa na mfanyabiashara aliyetakiwa kufanya hivyo.

Amesema mfanyabiashara huyo ambaye aliomba asitajwe jina lake,alifika kwenye eneo la mpaka wa Sirari unaopakana na nchi ya Kenya akiwa na lori lililokuwa na vifaa vya ujenzi ambapo baada ya kufanyiwa mahesabu na afisa huyo alitakiwa kulipa ushuru wa shilingi milioni 48. Luoga amesema baadae mfanyabiashara huyo alitakiwa na afisa huyo kulipa milioni 23 pekee kwenye mapato ya serikali na yeye awekewe kwenye akaunti ya mdogo  wake kiasi cha shilingi milioni 15 ili aweze kupitisha mzigo huo uliokuwa ukiingia nchini.

Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya kupata taarifa hizo alifanya uchunguzi kupitia akaunti hiyo namba 0152282620401 kwenye benki ya CRDB yenye jina la Lyimo Phanuel,ilikutwa na kiasi kikubwa cha fedha huku mtu huyo akiwa hana kazi yoyote ya kueleweka ya kuingiza fedha hizo.


Post a Comment