0


IKIWA ni kukabiliana na wagombea watakaoanza kufanya kampeni mapema na kujihsisha vitendo vya kutoa Rushwa ili wachaguliwe, Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara kimetoa ruksa ya kurekodiwa wagombea watakaofanya vitendo hivyo ili kuweza kupata ushahidi wa kuwaengua kuomba nafasi za uongozi.

Akizungumza na BLOG HIIofisini kwake katika kuelekea uchaguzi wa chama hicho, Katibu wa CCM mkoa wa Mara,Innocent Nanzabar, amesema wagombea wote waliomba nafasi za uongozi wamezuiwa kufanya kampeni kabla ya wakati na katika kukabiliana na hilo ni muhimu kubuni mbinu nyingi zaidi.

Amesema ili kupata ushahidi na kuchukua hatua kwa wagombea watakao kaidi ni wanachama wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya ngazi ya Kata na Wilaya wafatilie nyendo zao na kurekodi vitendo watakavyokuwa wanafanya ikiwa ni wao wenyewe au wapambe katika maeneo yao.

Nanzabar amesema wapo wagombea ambao wanajiamini kuwa majina yao yatarudi kutoka ngazi ya taifa na kuanza kupitapita kwenye Kata na wilayani ili kwenye uchaguzi wa mkoa waweze kuchaguliwa jambo ambalo maadili ya chama yanakatazwa kufanywa.

Amesema kutokana na maendeleo ya kimtandao wanachama wanaopingana na vitendo visivyofaa ndani ya chama wanapaswa kuwasaidia viongozi kwa kuwabaini wagombea hao kwa kuwarekodi ili kupata ushahidi wa kubaini makosa yao na kuenguliwa kwenye uchaguzi.

“Tunaomba wanachama wetu watusaidie ili kuweza kuwakamata wagombea ambao wanashindwa kufuata maadili na maelezo ya chama na hili kuwapata mtakapowaona muwarekodi tupate ushahidi na kupeleka panapo husika.

“Makatibu wa CCM kule kwenye ngazi ya wilaya pia wanapaswa kutusaidia kupata taarifa za wagombea hao kwa kuwa huko kwenye wilaya ndiko kunaweza kutokea vitendo vya kuanza kampeni mapema na kutolewa kwa Rushwa,”amesema Nanzabar.

Katibu huyo amesema jumla ya wanachama 24 wamejitokeza kuomba nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mara,19 wanawania nafasi ya halmashauri kuu ya taifa (NEC) na 16 wanawania nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ambao wametakiwa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.

Aidha amewataka wagombea wote kujiepusha na vitendo vyote vinavyokatazwa kwa kuwa pale watakapotolewa taarifa na zikathibitishwa wataenguliwa kugombea nafasi hiyo na hata kama watakuwa wamechaguliwa matokeo yao yatafutwa.

Amesema tayari alifanya ziara  kwa kushirikisha vyombo vya dola ikiwemo Takukuru na kutoa elimu yanayofaa kuzingatiwa kwa wagombea ikiwemo utoaji wa Rushwa hivyo atakaye jihusisha na vitendo vilivyokatazwa na kukamatwa asije kulalamika baada ya kuchukuliwa hatua.

Baadhi ya wagombea walioomba nafasi za uongozi ambao hawakutaka majina yao yaandikwe kwa kuwa bado hawajateuliwa na kukatazwa na kanuni,wamesema watazingatia yote yaliyokatazwa ili kuepuka kuondokewa na sifa za kugombea.



Post a Comment