DIWANI wa
Kata ya Kitaji katika manispaa ya Musoma, Frenk Wabare, ameliomba baraza la
madiwani la halmashauri hiyo kuacha kuongeza ushuru wa asilimia 40 kwa
wafanyabiashara wa soko kuu la Musoma kwa kuwa wanafanya biashara kwenye
mazingira magumu.
Akizungumza
kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kupitisa rasimu ya bajeti ya halmasauri
hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2018 hadi 2019, amesema mazingira ya soko sio mazuri
ikiwemo kushindwa kufanya biashara pale mvua inapokuwa inanyesha kutokana na
kutokuwa na miundombinu mizuri ya kutoa maji hivyo sio vyema kuwaongezea ushuru
wakati hawajafanyiwa marekebisho.
Amesema
amekuwa akikutana na wakati mgumu anapotembelea soko hilo ambalo lipo kwenye
Kata yake kutokana na malalamiko ya wafanyabishara na halitakuwa jambo la
busara kuwaongezea gharama za ushuru wakati mahitaji yao hayajatekelezwa.
Wabare
alisema ni vyema kwanza yakatekelezwa yale ambayo wafanyabiashara hao wamekuwa
wakiyalalamikia ndipo waweze kukaa nao chini kuona kama kutakuwa na sababu za
kuwaongezea gharama za ushuru ambazo wanatakiwa kuzilipa.
Diwani huyo
amesema nyakati za mvua maji yamekuwa yakijaa kwenye soko hilo na kuwafanya
kushindwa kufanya biashara na kuwaomba madiwani kwa kuwa soko hilo
linawahudumia wakazi wote wa manispaa ya Musoma ni vyema wakakubaliana na
maombi yake ya kutoongeza gharama za ushuru
Aidha diwani
huyo ameliomba baraza hilo kukubali kuhamisha fedha zilizotengwa kiasi cha
shilingi milioni 20 kwenye bajeti ya mwaka 2018-2019 kwaajili ya ujenzi wa duka
kubwa (super markert) kwenye bustani ya Malikia Elizaberth iliyopo eneo la
stend ya zamani na kuzipeleka kwenye ukarabati wa soko pamoja na ujenzi wa
nyumba ya kupumzika abiria.
“Naomba
tusiwaongezee gharama za ushuru hawa wafanyakazi wetu kutokana na mazingira ya
pale sokoni kutokuwa mazuri kwa sasa tujikite kwenye kuboresha baadae
tutazungumza nao kama kuna sababu za kuongeza gharama za ushuru.
“Lakini
nawaomba waheshimiwa madiwani tukubaliane na ombi langu zile fedha ambazo
zimetengwa kwaajili ya ujenzi wa duka kubwa pale kwenye bustani ya malikia
ziamishiwe kwenye ukarabati wa soko na jengo la abiria kupumzika pale kwenye
stend yetu,”alisema Wabare.
Kupitia
maombi ya diwani huyo, Meya wa manispaa ya Musoma, Patrick Gumbo, aliwahoji
madiwani wa halmashauri hiyo kama wanakubaliana na maombi hayo na kukubali kwa
pamoja kulidhia maombi ya diwani huyo ili kuondoa adha kwa wafanyabiashara wa
soko kuu pamoja na wasafiri.
Post a Comment
0 comments