0
SEHEMU YA WANAFUNZI NA WALIMU WA SHULE YA MSINGI MWISENGE

WANAHABARI WALIKUWA KARIBU KATIKA KUFATILIA TUKIO HILO

MENEJA WA HUDUMA KWA JAMII WA NHC MUUNGANO SAGUYA AKIZINDUA VYOO HIVYO

SAGUYA AKIZUNGUMZA NA WALIMU,WANAFUNZI PAMOJA NA WANAHABARI




SAGUYA AKITEMBELEA VYOO HIVYO

CHOO CHA ZAMANI SHULENI HAPO NA CHINI KILICHOJENGWA NA NHC

Na Shomari Binda
       Musoma,

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa msaada wa ujenzi wa jengo la vyoo lenye matundu 14 katika Shule ya Msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwa ni sehemu ya maazimisho ya Miaka 50 ya Shirika hilo.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Jengo hilo uliofanyika shuleni hapo,Meneja wa Huduma kwa Jamii wa Shirika hilo Muungano Saguya alisema Shirika la nyumba la Taifa kwa kutamba wajibu wake kwa Jamii linayo sera ya kusaidia Maendeleo ya Jamii katika Nyanja mbalimbali.

Alisema licha ya kuwepo changamoto mbalimbali katika Shule hiyo yenye historia kubwa katika Taifa la Tanzania wamejaribu kupunguza changamoto hizo kwa kubolesha miundombinu ya vyoo ambayo imeghalimu kiasi cha shilingi milioni 16 ili kuviweka katika hali ya kuridhisha.      

Saguya alisema ili mtoto aweze kupenda shule pamoja na masomo ni wajibu kumuwekea mazingira mazuri ambayo yatamfanya kila wakati atamani kwenda shuleni na kujiepusha na utoro ambao unaweza kuzolotesha elimu.

“Kila mmoja wetu anafahamu kuwa ili Nchi yoyote iendelee inahitaji elimu kwa watu wake,Taifa letu halikadharika limekuwa likijitahidi kuwekeza katika elimu ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko makubwa ya uchumi na teknolojia ya Dunia.

“Hivi sasa katika ukanda wa Afrika Mashariki tumeungana na Nchi jirani katika Nyanja za kiuchumi,hivyo itoshe kusema hatuwezi kushindana na Nchi hizi jirani kama tutapuuzia kuweka mkazo katika kuwekeza zaidi katika Elimu,”alisema Saguya.

Alisema NHC ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mahala pazuri pa kujistiri imeona itengeneze vyoo vya kisasa katika shule hiyo kwa kuwa shule isipokuwa na vyoo imara huwafadhaisha na kuwadhalilisha wanafunzi wengi.

“Shirika lina kila sababu ya kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere kama mnakumbuka NHC lilikuwa Shirika la kwanza kuanzishwa na Mwalimu Mwaka 1962 ikiwa ni Mwaka mmoja baada ya Uhuru.

“Mwalimu Nyerere alithamini sana vitu vitatu katika kuleta utu wa Mwanadamu vitu ambavyo ni pamoja na nyumba,mavazi na malazi hivyo tunatoa mchango huu kama shemu ya kuadhimisha miaka 50 na kuenzi jitihada za Mwalimu Nyerere la kulianzisha Shirika hili,”aliongeza.

Katika taarifa iliyotolewa na Meneja NHC Mkoa wa Mara Jocton Matogo juu ya ujenzi huo alisema ujenzi ulianza julai 2012 na kukamilika oktoba 2012 ikiwa na matundu saba kwa Wasichana na matundu saba kwa wavulana.  

Alisema  mradi wa choo cha wanafunzi katika shule hiyo uliibuliwa na uongozi wa Shirika Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na uongozi wa shule baada ya kutathimini mahitaji ya haraka na kutimiza sehemu ya miradi ya huduma ka Jamii inayotolewa na Shirika hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Mathias Buguti amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa msaada waliotoa katika shule hiyo kwa kuwa ilikuwa ni hitaji lao kubwa kwa sasa kwa kuzingatia wingi wa wanafunzi katika shule hiyo
.

 
  




Post a Comment